ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 8, 2024

“UJENZI WA NYUMBA ZA WAATHIRIKA WA MAAFA HANANG’ KUZINGATIA UBORA NA VIWANGO VINAVYOTAKIWA” DKT. YONAZI




Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa nyumba zinazotarajiwa kujenga kwa ajili ya waathirika wa maafa ya maporomoko ya tope na mawe kutoka mlima Hanang’ katika Wilaya ya Hanang’ mkoa wa Manyara yaliyotokea tarehe 3 Disemba, 2023 utazingitia ubora na viwango vinavyotakiwa ikiwa ni sehemu ya hatua ya kurejesha hali kwa waathirika hao.

Ameyasema hayo wakati wa kikao chake na timu ya Wataalamu kutoka SUMA JKT na Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania TRCS (RED CROSS) cha Kuwasilisha Mpango wa Ujenzi wa Nyumba kwa waathirika hao kilifanyika tarehe 03 Februari, 2024 katika Ukumbi wa Ofisi hiyo Jijini Dodoma.

Alieleza kuwa katika hatua za mzingo wa menejimenti ya maafa hatua zote ni muhimu ikiwemo ya kurejesha hali hivyo ni wakati sahihi kuitendea haki hatua hiyo kwa kuzingatia ubora zaidi kwa kulinganisha hali ya awali.

“Ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea na kuratibu na kusimamia shughuli za kurejesha hali kutokana na maafa ya Hanang’, miongoni mwa kazi zinazotekelezwa katika kurejesha hali ni ujenzi wa nyumba 108 kwa wale wote waliofanyiwa tathmini mara baada ya nyumba hizi kubomoka na zilizo katika hali hatarishi,” alieleza

Aliongezea kuwa hadi sasa tayari timu ya wataalam ya Usimamizi wa Mradi kwa kushirikiana na timu ya Wataalam wa SUMA JKT imekamilisha mapendekezo ya maandalizi ya hatua za ujenzi huo.

Dkt. Yonazi aliwashukuru kwa namna walivyojitoa na kuwa tayari kuunga mkono jitihada za Serikali katika hatua hiyo muhimu ya kurejesha hali kwa waathirika wa maafa Wilayani humo.

Wakiwasilisha taarifa ya Mpango wa Ujenzi wa Nyumba hizo kwa wakati tofauti Mkurugenzi Mtendaji wa SUMAJKT Kanali Petro Ngata pamoja na Mhandisi Ernest Mbuya kutoka Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania -RED CROSS wamesema watashirikiana katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi huo ili kukamilisha kwa wakati na viwango vilivyokubaliwa.

Aidha walieleza kuwa, wamejipanga kushirikiana na kukamilisha nyumba hizo ili kuhakikisha waathirika wa maafa hayo wanarejea katika hali nzuri ya maisha yao na kuendelea na shughuli za kujiletea maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

No comments: