Na Baraka Messa, Songwe
JESHI la polisi mkoani Songwe katika kuimarisha ulinzi na usalama kwa kushirikisha jamii limefanikiwa kuwakamata watu watatu kwa tuhuma za kupatikana na nyara za serikali vipande 9 vya meno ya tembo vya thamani ya kilo 20 bila kuwa na kibali.
Akizungumza Januari 1/2024 na waandishi wa habari,kaimu kamanda wa polisi mkoani Songwe,Kamishna msaidizi wa jeshi hilo,ACP-Gallus Hyera ameeleza kuwa jeshi limewashikilia watuhumiwa hao kwa kukutwa na meno 9 ya tembo.
Alisema watuhumiwa hao ambao majina yao yamewehifadhiwa kwa ajili ya kutoharibu upelelezi,walikamatwa Januari 30/2024 na wengine januari 31/2024 katika msako uliofanywakijiji cha Ibembwa kata ya Igamba wilayani Mbozi.
Alisema watuhumiwa hao walikutwa wameficha meno 9 ya tembo kwenye begi ambalo mmoja wapo aliweka ndani ya mfuko wa Sandarusi akiwa kwenye harakati za kutafuta wateja huku thamani yake bado haijajulikana.
Aidha alisema kuwa katika upelelezi wa awali umebaini kuwa watuhumiwa ni wawindaji haramu wasafirishaji na wauzaji wa nyara za serikali,ambapo watafikishwa mahakamani uchunguzi utakapobainika.
Alisema jeshi la polisi linatoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Songwe wanaojihusisha na uhalifu wa nyara za serikali na ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto kuacha mara moja kwani hawataweza kukwepa mkono wa sheria.
Aliongeza kuwa watuhumiwa hao hawajaweza kutajwa majina yao kwa kuwa wapo kwenye uchunguzi zaidi na iwapo watatajwa majina washirika wao ambao wanatafutwa wataweza kukimbia na wao kushindwa kuwakamata.
Alisema uchunguzi ukikamilika watapelekwa mahakamani kujibu mashitaka yao .
No comments:
Post a Comment