Serikali ya Tanzania imeipongeza Serikali ya Ethiopia kwa kuweka historia kwa kuwa nchi ya kwanza kujenga majengo ya Ofisi na Makazi ya Balozi katika Mji wa Serikali Dodoma na kutoa wito kwa nchi nyingine kuiga mfano huo.
Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk kupitia kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethipia, Mhe, Birtukan Ayano ambapo kwa pamoja waliweka Jiwe la Msingi la ujenzi huo kwa niaba ya Serikali zao katika hafla iliyofanyika Mtumba jijini Dodoma leo Mei 17, 2024.
Balozi Mbarouk alieleza kuwa uwekaji wa jiwe la msingi huo ni kielelezo tosha cha kuimarika kwa ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Ethiopia ambao ulianza tangu enzi za waasisi wa mataifa haya, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Haile Selassie.
Kwa upande wake, Mhe. Ayano alisema uwekaji wa jiwe la msingi huo ni ishara ya ushirikiano mzuri uliopo baina ya nchi hizi mbili na dhamira ya dhati ya Serikali ya Ethiopia ya kuuimarisha zaidi, hususan katika nyanja ya biashara na uwekezaji.
Hafla ya uwekaji jiwe la msingi ilihudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule ambapo aliwahakikishia jumuiya ya wanadiplomasia nchini kuwa Dodoma ipo tayari kuwapokea na miundombinu ya kijamii ikiwemo maji, elimu, afya na usafirishaji, Serikali inaendelea kuijenga na kuiboresha iliyopo.
Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Ummy Nderiananga; Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Vicent Mbogo, Naibu Katibu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Mussa, Balozi wa Ethiopia nchini, Mhe. Shibru Mamo Kedida, Meya wa Halimashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe na viongozi waandamizi wa Serikali.
No comments:
Post a Comment