Advertisements

Friday, June 14, 2024

RAIS SAMIA ATOA SHILINGI MILIONI 900 UPASUAJI WA MOYO WATOTO JKCI



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi milioni 900 kwaajili ya kuwasaidia watoto wenye matatizo ya moyo wasiokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu.
Fedha hizo zimelenga kuwagharamia watoto wenye magonjwa ya moyo ambayo ni magumu kufanyiwa upasuaji ambao wamekuwa katika foleni ya kusubiria matibabu katika Taasisi Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Akizungumza na mwandishi wa habari hii hivi karibuni jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alisema fedha hizo zitatumika kuwafanyia upasuaji wa kufungua kifua watoto 30 matatibu yatakayotolewa kwa kipindi cha wiki mbili na wataalamu wa Taasisi hiyo.


“Tunashukuru tangu tumeanza kambi hii imekuwa ya mafanikio kwani upasuaji tunaoufanya ni mkubwa kwa watoto, kupitia kambi hii pia tumeweza kumfanyia upasuaji mtoto mwenye uzito wa kilo mbili na upasuaji wake umefanikiwa”, alisema Dkt. Angela.

Dkt. Angela alisema matibabu yanayotolewa kwa watoto hao 30 ni makubwa kwani watoto wana changamoto zaidi ya moja zinazopelekea mahitaji ya vifaa tiba na dawa kuwa makubwa na kuyafanya matibabu hayo kuwa na gharama kubwa.

“Tunamshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa moyo wake wa kujitoa kwaajili ya watoto hawa ambao wanapata huduma katika Taasisi yetu”, alisema Dkt. Angela.

Kwa upande wake Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Felix Shonyela alisema kambi hiyo inatoa huduma kwa watoto wenye matatizo magumu na wale wenye shida zaidi ya moja kwenye mioyo yao.

“Baada ya kufanyiwa upasuaji wa moyo watoto hawa wataendelea kufanya shughuli zao kama kawaida na shida waliozokuwa wanapata mwanzo zitaondoka na kuwa vizuri kama watoto wengine”, alisema Dkt. Shonyela.

Dkt. Shonyela alitoa wito kwa wazazi wenye watoto wanapoona watoto wana dalili za kuchoka, vidole kuvimba, kuwa na rangi ya bluu kwenye vidole na midogo pamoja na ukuaji hafifu kuwafikisha JKCI mapema kwaajili ya uchunguzi kwani watoto wengi wamekuwa wakicheleweshwa na kupelekea baadhi ya matibabu kushindwa kufanyika.

Naye mzazi wa mtoto aliyefanyiwa upasuaji katika kambi hiyo Prisca Theophil alimshukuru Rais Samia kwa kuwasaidia watoto wenye matatizo ya moyo wanaotoka katika familia zenye uwezo mdogo kiuchumi akiwemo mtoto wake.

Prisca alisema aligundua mtoto wake ana tatizo la moyo mwaka 2022 na kuanza kupatiwa matibabu JKCI lakini hakuwa na uwezo wa kulipia gharama za upasuaji kutokana na kipato chake kuwa kidogo.

“Namshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia kwa kuwasaidia watoto wetu, mwanangu alikuwa na tundu kwenye moyo, matatizo ya valvu na tatizo la mishipa ya damu kupitia fedha za mama Samia amefanyiwa upasuaji na sasa anaendelea vizuri”, alisema Prisca.

No comments: