Advertisements

Wednesday, June 12, 2024

UBADHIRIFU WA KUTISHA MSIKITINI JIJINI MWANZA



Na Mwandishi Wetu, Mwanza
WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini nchini (RITA), imebaini ubadhirifu mkubwa wa kiasi cha shilingi bilioni moja za Kitanzania katika Msikiti wa Ijumaa uliopo Jijini Mwanza na hatua za kisheria zimeshaaza kuchukuliwa.

Akizungumza wakati wa ziara yake mkoani Mwanza mwishoni mwa wiki, Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Bw Frank Kanyusi aliwaambia waumini wa msikiti huo kuwa ziara yake ili lenga kuwasilisha ripoti ya ubadhirifu wa fedha kwa waumini sambamba na kusimamia uchaguzi wa wasimamizi watakao simamia kwa muda mali za waumini wa msikiti.

“Rai yangu kwa wajumbe wa Bodi ya Udhamini wahakikishe wanatekeleza majukumu yao kama Sheria inavyowaelekeza au kuwataka na waelewe kuwa wao siyo wamiliki wa mali bali ni wasimamizi wa mali kwa niaba ya wanachama hivyo wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria ili kuzuia vitendo visivyofaa,” amesema Kanyusi.

Kwa mujibu wa Kabidhi Wasii Mkuu huyu, Februari 2 mwaka huu mwaka huu aliunda Kamati ya Uchunguzi ambayo ilifanya kazi kwa kipindi cha mwezi mmoja na ikaja na ripoti iliyoonyesha ubadhirifu wa fedha takribani shilingi bilioni moja za msikiti,

“Hatua za kisheria zimeanza kuchukuliwa sambamba na wale wote waliohusika kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria. RITA imewatoa hofu waumini wote kuwa mali zote za waumini wa msikiti zipo kwenye mikono salama,” amesema.

Kufuatia ubadhirifu na mivutano miongoni mwa baadhi ya waumini, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma ilielekeza iundwe kamati ya wasimamizi kabla ya Juni 20 mwaka huu, itakayosimamia mali zote za waumini wa Msikiti wa Ijumaa Mwanza.

Kwa upande wake, Afisa Sheria wa RITA, Emmanuela Mwingira amesema RITA imeshafanyia kazi marekebisho ya Katiba na kuchagua waumini kadhaa wa msikiti huo watakaofanya uchaguzi ili kupata bodi ya wadhamini.

“Kazi tuliyokuwa nayo ni pamoja na kupitia sheria yao na kufanya maboresho ili kuzuia makosa kutojirudia siku za mbeleni,” amesema Mwingira na kupongeza utulivu na ushirikiano uliotolewa wakati wote wa kikao na waumini wa msikiti.

Naye Muumini wa Msikiti huo, Sherally Sherally amesema sheria isipofuatwa haki haitopatikana na kuiomba RITA kuhakikisha kuwa wale wote waliohusika na ubadhirifu wanachukuliwa hatua stahihiki pamoja na kufikishwa mahakama.

Tukiendelea kuwachekea watu wanaojilimbikizia mali za waumini hatutafika mbali sambamba hilo pia wale tutakaowachagua watafanya hivyo hivyo kwani watajua hakuna tutakachowafanya,” amesema Sherally na kuiomba serikali kupitia mahakama kuchukua hatua kali za kisheria na kutoa fundisho kwa wengine.

Muumini huyo, alionyesha imani yake kwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassani katika kushughulikia na kutatua kero na changamoto zilizowasilishwa kwa kufanyiwa kazi na kupatiwa ufumbuzi wa kudunu.

Muumini mwingine Abdallah Tawfique mbali ya kuipongeza RITA hatua iliyozichukua, aliishukukuru pia serikali ya awamu ya sita kwa kufanya kazi kwa karibu na viongozi wa taasisi zote za dini na madhehebu mbalimbali hapa nchini.

Bodi ya kwanza ya udhamini ya msikiti huo ilivunjwa na serikali mwaka 2020 na baadaye kuundwa kwa Kamati ya mpito ya wajumbe kumi na watatu ambayo nayo imevunjwa na Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma kufuatia mvutano wa baadhi ya waumini uliokuwa unaendelea.

No comments: