Thursday, July 18, 2024

DC KILAKALA AHIMIZA USIMAMIZI WA MIRADI KUKAMILIKA ILI KUMUUNGA MKONO RAIS


Mkuu wa Wilaya ya Pangani Mussa Kilakala akizungumza na kutowa wito huo katika Kata ya Masaika wilayani humo alipotembelea kujagua miradi mbalimbali sambamba na kufanya mkutano wa hadhara kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Wananchi wa Kata ya Masaika Wilayani Pangani wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Pangani Mussa Kilakala, wakati wa ziara yake kutembelea na kukajua miradi mbalimbali sambamba na kufanya mkutano wa hadhara kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Na Hamida Kamchalla, PANGANI.
WATENDAJI wanaosimamia miradi yote ya maendeleo katika Wilaya ya Pangani wametakiwa kila mmoja katika eneo lake kuhakikisha miradi hiyo inasimamiwa kwa viwango vinavyokusudiwa ikiwa ni pamoja na kikamilika kwa wakati na kutoa huduma iliyokusudiwa kwa wananchi.

Mkuu wa Wilaya ya Pangani Mussa Kilakala ametoa wito huo katika Kata ya Masaika wilayani humo alipotembelea kujagua miradi mbalimbali sambamba na kufanya mkutano wa hadhara kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

"Miradi hii inapaswa kusimamiwa vizuri ili kuhakikisha inakamilika katika kiwango cha ubora na kwa wakati uliopangwa ili kuendana na mpango wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuleta fedha kwenye Wilaya hiyo kwajili ya maendeleo ya wananchi" amesema.

Katika ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ametembelea na kukagua ujenzi wa miundombinu ya usafi chini ya program ya uendelevu wa usambazaji wa maji na usafi wa mazingira vijijini (SRWSSP) katika zahanati ya Masaika ambao umepokea kiasi cha sh milioni 49.

Miradi iliyokaguliwa ikiwa katika hatua za utekelezaji inahusisha ujenzi wa choo cha mashimo matatu kwa ajili ya wagonjwa, ukarabati wa choo cha mashimo mawili kwa ajili ya watumishi, ujenzi wa kichomea taka, shimo la kutupia kondo la nyuma, shimo la kutupia majivu, ujenzi wa kinawia mikono, ujenzi wa mnara wa tanki la maji na uingizaji wa maji katika jengo la zahanati.

Sambamba na mradi huo katika zahanati ya Masaika Mkuu wa Wilaya alifika katika Kijiji cha Kigurusimba na kukagua ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya Masaika ambayo ilipatiwa fedha za ujenzi kiasi cha zaidi ya sh milioni 584 kupitia mradi wa kuboresha elimu ya sekondari (SEQUIP).

"Miundombinu iliyojengwa katika shule hii ilihusisha; ujenzi wa nyumba nane, vyumba vya madarasa, jengo la Utawala, vyumba vitatu vya maabara za sayansi, jengo la maktaba, jengo la TEHAMA na vyoo matundi 11, ambapo matano ya wavulana na sita ya wasichana matundu kwa ajili ya wanafunzi,

"Pamoja na fedha hizo shule hii pia imepokea fedha kiasi cha sh milioni 98 kupitia mradi huu wa kuboresha elimu ya sekondari kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu mbili kwa moja ikiwa na vyumba vitatu kila moja ambapo taratibu za kumpata fundi zinakamilishwa" amesisitiza Kilakala.

Hata hivyo Kilakala amewapongeza wananchi kwa kushiriki katika ujenzi wa shule hiyo ikiwa ni ishara ya kuunga mkono dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha elimu katika Wilaya ya Pangani.

No comments: