Thursday, October 17, 2024

MAKAMU WA PILI WA RAIS AZINDUA MITAMBO YA KUZALISHA GESI - HOSPITALI YA LUMUMBA


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Mitambo ya uzalishaji wa Hewa Tiba(Oxygen Plants) uliofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mjini Magharibi - Lumumba….
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Viongozi wa Wizara ya Afya, wawakilishi kutoka mashirika mbali mbali, watendaji wa Wizara ya Afya na wananchi waliohudhuria katika ufunguzi wa Mitambo ya uzalishaji wa Hewa Tiba (Oxygen Plants) uliofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mjini Magharibi - LUMUMBA.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla amesema Uwepo wa Mitambo ya uzalishaji wa Hewa Tiba (OXYGEN PLANTA) katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa Lumumba itaondoa kadhia na usumbufu wa utoaji wa huduma kwa wagonjwa katika hospitali zote za Serikali na Binafsi zilizopo hapa nchini.

Ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Mitambo ya kuzalisha Hewa Tiba (Oxygen Plants) katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mjini Magharibi LUMUMBA,

Makamu wa Pili wa Rais amesema hatua ya kufungwa Mitambo hio itarahisisha utoaji wa huduma kwa wagonjwa na kupunguza gharama ya ununuzi na usafirishaji wa hewa tiba hio amboyo ilikuwa ni kikwazo kikubwa kwa wagonjwa.

Amesema huduma ya HewaTiba itakayozalishwa hospitalini hapo itasambazwa katika hospitali mbali mbali za Serikali na binafsi ili kuhakikisha wananchi wanapata matibabu bora na ya kisasa na kufikia malengo ya Serikali ya kutoa huduma zilizobora kwa wananchi wote wa Zanzibar kuanzia ngazi ya Wilaya hadi Taifa.

Makamu wa Pili wa Rais amefahamisha kuwa Serikali ya Awamu ya Nane (8) imekuwa ikifanya juhudi kuhakikisha Sekta ya Afya inakuwa na madaktari bingwa na vifaa vya kisasa vya kutolea matibabu bora kwa wananchi jambo ambalo linaakisi Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2050 inayolenga kudumisha mfumo wa upatikanaji wa huduma za Afya zenye wataalamu bingwa, teknolojia na vifaa vya kisasa vya utabibu.

Aidha, Mhe. Hemed amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya itaendelea kuweka mazingira bora ya utoaji wa huduma ikiwemo kuifanyia ukarabati hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja, kuendelea na ujenzi wa vituo vya Afya, kuimarisha upatikanaji wa vifaa tiba sambamba na kukamilisha ujenzi wa nyumba za wafanyakazi wa sekta ya Afya ili waweze kukaa karibu na sehemu zao za kazi.

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais amewataka watendaji wa Wizara ya Afya ambao watakuwa na jukumu la kuiendesha mitambo hio kuhakikisha wanaitunza na kuifanyia matengenezo kwa wakati uliowekwa na kuitumia kwa uangalifu mkubwa kulingana na maelekezo sahihi ya utumiaji wa mitambo hio.

Nae Waziri wa Afya wa Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazurui amesema kuzinduliwa kwa Mitambo ya Hewa Tiba katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Lumumba kutasaidia kupunguza gharama za ununuzi na usafirishaji wa Oxygen pamoja na kupunguza changamoto ya kukosekana kwa huduma hio.

Mhe.Mazurui amesema upatikanaji wa hewa tiba hio utaamsha ari, kasi na nguvu ya ufanyaji kazi kwa wahudumu wa Afya katika kutoa huduma bora kwa wagonjwa sambamba na kuwashukuru wafadhili na wasimamizi wote waliosaidia kufanikisha kufungwa kwa mitambo hio wakiwemo wafadhili wakuu Global Fund kwa kutoa ushirikiano uliopelekea kukamilika kwa wakati ufungajibwa mitabo hio na kwa ubora wa hali ya juu.

Mhe. Mazurui ametoa maelekezo kwa wahudumu wa mitambo hio kuitunza na kuifanyia matengenezo kwa wakati uliopangwa ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuendelea kutoa huduma bila ya kusita.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka Gobal Fund BIBI SARA ASIMWE ameshukuru kwa kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa Serikali ya Zanzibar katika kipindi chote cha maadalizi ya ufungaji wa Mitambo hio hadi kufikia hatua ya kuikabidhi Serikalini kwa ajili ya kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Bibi Sara amesema mitambo hio ya hewa Tiba imezingatia ubora na uhitaji wa walengwa ambapo itaweza kutoa huduma kwa Zanzibar nzima kwa kila hospitali itakayokuwa na uhitaji wa tiba hio.

Mitambo hio ya kuzalisha Hewa Tiba imegharimu zaidi ya dola laki nane ambazo zimetolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Global Fund ambao ndio wafadhili wakuu wa mradi huo.

Imetolewa na kitengo cha Habari (OMPR )

No comments: