Thursday, October 10, 2024

NAIBU WAZIRI CHUMI ASISITIZA WELEDI NA UWAJIBIKAJI


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Mb.) akifungua mafunzo ya siku nne (4) ya Mawasiliano ya Kidiplomasia kwa Maafisa Waandamizi wa Wizara hiyo yanayofanyika katika Hotel ya St. Gaspar jijini Dodoma kuanzia tarehe 8 hadi 11 Oktoba 2024.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Bi. Chiku Kiguhe akimkaribisha Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi kwenye ufunguzi wa mafunzo ya Mawasiliano ya Kidiplomasia kwa Maafisa Waandamizi wa Wizara hiyo yanayofanyika katika Hotel ya St. Gaspar jijini Dodoma.
Katibu wa Mabalozi Wastaafu, Balozi Bertha Semu Somi akisisitiza jambo kwenye ufunguzi wa mafunzo ya Mawasiliano ya Kidiplomasia kwa Maafisa Waandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki yanayofanyika katika Hotel ya St. Gaspar jijini Dodoma.
Balozi Peter Kalaghe akifuatilia mafunzo Maafisa Waandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akifuatilia hafla ya ufunguzi wa mafunzo ya Mawasiliano ya Kidiplomasia kwa Maafisa Waandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki yanayofanyika katika Hotel ya St. Gaspar jijini Dodoma.
Mafunzo yakiendelea
Picha ya pamoja


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Mb.) amewasisitiza Maafisa Mambo ya Nje Waandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuongeza uchapakazi na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Hayo yamejili wakati wa hafla ya ufunguzi wa mafunzo ya siku nne (4) ya Mawasiliano ya Kidiplomasia kwa Maafisa Waandamizi wa Wizara hiyo yanayoendelea katika Hotel ya St. Gaspar jijini Dodoma kuanzia tarehe 8 hadi 11 Oktoba, 2024.

Akiongea katika ufunguzi huo Mhe. Chumi ameeleza furaha yake kuwaona Mabalozi Wastaafu wakiendelea kushirikiana na Wizara na kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa Wizara kila wanapohitajika au kuombwa kufanya hivyo.

Mafunzo hayo yanalenga pamoja na masuala mengine kuwajengea uwezo watumishi katika utekelezaji wa majukumu yao kwa ufasaha kwa kuwa wao ni kiungo muhimu katika kutekeleza jukumu la msingi la Wizara la kuratibu masuala ya kikanda na kimataifa kwa niaba ya Serikali.

‘’Katika mafunzo haya ya mawasiliano ya kidiplomasia mtajifunza kukusanya taarifa, kuchambua taarifa na kutunza siri za serikali kwa maslahi ya taifa, hivyo natarajia yatakuwa chachu katika kuongeza ufanisi na uwajibikaji’’, alisema Mhe. Chumi.

Mabalozi hawa ni watumishi waliomaliza muda wa utumishi wa umma lakini wameiishi na kuitekeleza diplomasia kwa vitendo, hivyo ni vema mkawa makini kufuatilia na kuyapokea mafunzo mnayopewa kwa umakini. Pia akaongeza kuwa naye ni zao lililotengenezwa na Mabalozi wanaotoa mafunzo hayo na akawashukuru kwa malezi yao na kwa kuendelea kuisaidia wizara na Serikali kwa ujumla.

Ameeleza pia mafunzo hayo yatainua utendaji wa Wizara kwa kuwa idadi kubwa ya watumishi wapya watapata fursa ya kupata ujuzi zaidi wa namna ya kutekeleza Sera ya Mambo ya Nje inayotilia msisitizo wa utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi.

Naye Katibu wa Mabalozi Wastaafu, Balozi Bertha Semu Somi ameeleza kuwa jukumu hilo la kuwajengea uwezo watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwao ni fahari kwa kuwa ni kielelezo kuwa bado wanamchango katika kuendelea kusaidia Serikali.

“Serikali iliwekeza katika kutujengea uwezo wa kutekeleza kwa ufasaha majukumu ya kidiplomasia hivyo, nasi tunapata nafasi ya kurejesha kile kilichowekezwa kwetu kwa vijana ambao wanarithishwa jukumu hili muhimu kwa maslahi ya nchi’’ alisema Balozi Somi.

Pia ameeleza maafisa wanaonesha umakini kwa kuwa katika siku ya pili kila Afisa amefanya wasilisho ya yale yaliyotangulia kufundishwa ambapo ametoa mrejesho mzuri kwa Mabalozi wanaofundisha katika kufahamu nini kimepungua na nini kiongezwe katika kuyaboresha mafunzo hayo.

Maafisa wanaohudhuria mafunzo wamesisitizwa kujiongezea weledi kwa kusoma sera, sheria na miongozo mbalimbali na pia wasome nyaraka kama Sera ya Mambo ya Nje, Diara ya Maendeleo ya Taifa, Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Mkataba wa Vienna, Kanuni za Utumishi wa Mambo ya Nje, na miongozo mingine ya kikanda na kimataifa.

No comments: