Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO Tanzania Profesa Hamis Malebo akiwa katika picha ya pamoja baadhi ya Watendaji wa Serikali ya Tanzania katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa unaoenedelea New York Marekani.
Na Mwandishi Wetu,New York Marekani.
Katibu Mtendaji wa Tume ya UNESCO Tanzania Profesa Hamisi M. Malebo amesema Serikali ya Tanzania imeweka kipaumbele katika kulinda mifumo ya uhifadhi wa ikolojia iliyomo katika ardhi ya Tanzania.
Prof Malebo amesema pamoja na ukweli kuwa jamii ya Wamaasai imeishi pamoja na wanyamapori kwa vizazi vingi, zipo taarifa za changamoto za kiikolojia na migogoro hatarishi kati ya wanadamu na wanyamapori na kwa nia njema, serikali iliwahusisha wananchi wa Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto za kiusalama, uchumi wa wenyeji na kulinda ikolojia ya eneo la hifadhi bila kuvunja haki za watu wanaoishi ndani ya maeneo hayo.
Profesa Malebo ameyasema hayo akizungumza katika Kikao cha Kamati ya Tatu ya Masuala na Haki za Watu wa Asili katika mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaoendelea jijini New York nchini Marekani.
Amesema Tanzania inao mfumo wake wa ndani wa sheria na imejiwekea utaratibu wa masuala ya ardhi yenye lengo la kulinda umoja na amani nchini.
Amesema mfumo wa umiliki wa ardhi Tanzania umekuchukua tahadhari ya uwezekano wa mgawanyiko wa kijamii na hivyo kuacha ardhi kuwa mali ya umma aliyokabidhiwa Rais kama mdhamini.
Prof. Malebo amesema ili kufanikisha hilo serikali ya Tanzania imeweka mfumo wa kisheria kupitia Sheria ya Ardhi ya 1999 na Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya 1999, ambapo ardhi ni mali ya taifa. Prof. Malebo alifafanua kuwa, "Tanzania haikubaliani na dhana ya 'watu wa asili' ambayo pia inapingwa na mataifa kadhaa ya Afrika, Asia na Ulaya.
Prof. Malebo ameukumbusha mkutano huo kuwa Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ni eneo la urithi wa dunia la UNESCO.
Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko la watu na shughuli za kibinadamu ambazo zinaleta tishio kwa mfumo wa ekolojia wa eneo hilo, hasa katika juhudi za kuhifadhi wanyamapori na mimea ya asili.
Hata hivyo amesema mapitio ya matumizi mseto ya ardhi yaliyowahusisha wananchi wa Ngorongoro kwa muafaka walipendekeza kuhama kwa hiari ili kulinda mazingira na kuimarisha maisha ya jamii za maeneo hayo.
Prof. Malebo amesema wakati akifafanua umuhimu wa wananchi kuhama kwa hiari toka Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro alieleza kuwa, mfumo wa ikolojia wa Serengeti-Mara ni wa pekee na ndiyo pekee uliobakia duniani unaoonesha maajabu ya asili ya uhamiaji wa wanyama pori, maarufu kwa uhamiaji mkubwa wa nyumbu, pundamilia, na wanyama wengine wakienda kwa mzunguko kutokea Serengeti kupitia Ngorongoro, Loliondo na kuingia Maasai-Mara ya Kenya halafu wanarudi tena Serengeti.
Kuulinda mfumo huu muhimu kwa ulimwengu ni jukumu la Tanzania na mataifa yote ya dunia. Makazi na shughuli za binadamu ndani ya hifadhi yamekuwa yanasababisha migogoro juu ya matumizi ya ardhi kati ya binadamu na wanayamapori kwa mfano, kilimo, malisho ya mifugo, kutafuta kuni na dawa asili yamekuwa yanasababisha wananchi kujeruhiwa au kuuawa na wanayamapori na kuwepo migogoro kati ya binadamu na wanyamapori yamekuwa ni masuala ya kawaida Ngorongoro.
No comments:
Post a Comment