ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, November 3, 2026

TANAPA YAWEKA HISTORIA UGALLA: MRADI WA UMEME WA SHILINGI MILIONI 380.2 KUCHOCHEA MAENDELEO YA JAMII NA UTALII UGALLA

 

Na. Hance Mbena - Tabora


Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Novemba 02, 2026 limezindua mradi wa umeme katika Hifadhi ya Taifa Mto Ugalla uliogharimu kiasi cha shilingi milioni 380.2 za kitanzania, mradi utakaochochea maendeleo ya utalii, uhifadhi, uwekezaji pamoja na maendeleo kwa jamii zinazozunguka hifadhi hiyo.

Mradi huo umezinduliwa na Kamishna wa Uhifadhi TANAPA Massana Mwishawa ambapo alibainisha kuwa, mradi huo wa umeme unatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo kwa wananchi wa kijiji cha Uyumbu kinachopakana na hifadhi, sambamba na kuboresha utoaji wa huduma kwa watalii na kuboresha maisha ya watumishi kwa kupata nishati ya umeme. 

Akizungumza katika Uzinduzi huo Kamishna Mwishawa alisema "mradi huu umelenga kuchochea shughuli za utalii na kuwavutia wawekezaji kuwekeza hifadhini kwa kuwasogezea na kuwarahisishia upatikanaji wa nishati ya umeme pamoja na kuwa chachu ya jamii kuanzisha shughuli mbalimbali za uzalishaji zinazotokana na matumizi ya umeme na kujitengenezenea kipato".

Aidha, Mkuu wa Kanda ya Magharibi TANAPA, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Godwell Meng’ataki  alisisitiza upatikanaji wa umeme unatarajia kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa wananchi pamoja na kuchochea shughuli za maendeleo. Hatua hiyo pia itasaidia kuimarisha huduma kwa watalii, kuongeza uzoefu kwa watalii na kuchangia ukuaji wa sekta ya utalii katika Hifadhi ya Taifa Mto Ugalla.

Naye, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mto Ugalla, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Moronda Moronda ametoa shukrani kwa TANAPA kwa kufadhili na kutekeleza mradi wa kimkakati wa usambazaji wa umeme wenye thamani ya Shilingi milioni 380.2, alieleza kuwa mradi huo ni hatua kubwa katika kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi na kuongeza hamasa katika utoaji wa huduma kwa watalii na kuongeza pato la Taifa. 

Mradi huo umehusisha uwekaji wa nguzo 96 za zege pamoja na transfoma moja yenye uwezo wa KVA 100 zitakazowezesha upatikanaji wa umeme na kuimarisha mifumo ya uendeshaji na ufanisi wa shughuli mbalimbali na ndani ya hifadhi.

TANAPA inaendelea kutekeleza dhamira yake ya kuunganisha uhifadhi na maendeleo ya jamii kwa kuwekeza katika miradi ya kimkakati yenye manufaa ya muda mrefu. Mradi huu ni kielelezo cha namna uwekezaji katika miundombinu unavyoweza kuleta matokeo chanya kwa jamii, kuboresha huduma za utalii na kuimarisha uhifadhi endelevu kwa manufaa ya Taifa.









No comments: