ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 17, 2010

Ufaransa yatoa sh mil 100 kwa wananchi Kilosa


BALOZI wa Ufaransa nchini, Jacques de Labriolle, leo amekikabidhi msaada Chama Cha Msalaba Mwekundu tawi la Tanzania, wenye thamani ya takribani Sh milioni 100 za Tanzania kwa kuwasaidia waathirika wa mafuriko wilayani Kilosa katika mkoa wa Morogoro.

Balozi Labriolle amesema, Serikali ya Ufaransa imetoa Euro 50,000 kuzisaidia zaidi ya familia 200 zilizokumbwa na mafuriko Kilosa.

“Mwezi uliopita, mara moja baada ya maafa haya, Chama Cha Msalaba Mwekundu Ufaransa kimetuambia kwamba hali katika wilaya ya Kilosa ilikuwa mbaya sana na kimetupa ushauri kuitikia ombi la msaada wa dharura lililotolewa na Chama Cha Msalaba Mwekundu Tanzania” amesema Balozi huyo katika hotuba aliyoitoa kwa lugha ya Kiswahili.

Amesema, fedha hizo zimetumika kununua vifaa vya kuwasaidia waathirika wa Kilosa, vikiwemo vyandarua, vyombo vya kupikia, mahema, dawa za kusafisha maji ya kunywa, na pia kugharamia usambazaji wa maji safi kwenye maeneo yaliyokumbwa na mafuriko.

“Chama Cha Msalaba Mwekundu Tanzania kitafanya kazi kwa karibu na mamlaka zilizo katika wilaya ya Kilosa ili kuhakikisha kuwa misaada inawafikia watu walioathirika zaidi katika wilaya hiyo” amesema Balozi Labriolle na kubainisha kwamba hivi karibuni atakwenda kwenye maeneo yaliyokumbwa na mafuriko Kilosa kuona hali ilivyo.

“Kama mnavyojua, mvua kubwa zilizonyesha kati ya mwezi Desemba mwaka jana na Januari mwaka huu zimesababisha mafuriko makubwa nchini Tanzania hasa katika Wilaya ya Kilosa” amesema. 

1 comment:

Anonymous said...

kufa kufaana,haya ulaji huo!!!