ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 16, 2010

Mwamba wafunika wachimbaji mgodini

WATU watatu wanasadikiwa kupoteza maisha baada ya mwamba kuporomoka kwenye mgodi wa Bulyanhulu, wilayani hapa.

Shughuli za uchimbaji zimesimamishwa ili kupisha jitihada za uokoaji zilizoanza tangu ajali hiyo ilipotokea kati ya saa 8 na saa 9 alfajiri ya kuamkia jana.

Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa Kampuni ya African Barrick Gold inayomiliki mgodi huo, Teweli Teweli, jana aliiambia HabariLeo, kwamba kati ya wafanyakazi hao wa mgodi ambao awali sauti zao zilisikika wakiwa ndani ya kifusi, mmoja wao alikuwa akiendesha mashine aina ya Jumbo kabla ya tukio.

Hadi jana saa 9 alasiri, kikosi cha uokoaji cha mgodi huo kilikuwa kikiendelea kuwasaka wafanyakazi hao bila mafanikio. Wanaoaminika kufukiwa katika kina cha meta 900 ni Dickson Kaderema (dereva wa Jumbo), Joel Martin na Vedastus Tanbise.

Taarifa zilisema awali kulikuwa na wafanyakazi 30 ndani ya mgodi lakini walinusurika. Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya wakazi wa maeneo yanayozunguka mgodi huo, walisema vijiji vya Kakola, Bugarama na Ilogi, vilitawaliwa na hekaheka baada ya kusikia taarifa hizo.

Kulikuwa na vilio kutoka kwa ndugu wa wafanyakazi hao waliokuwa kwenye kifusi. Alisema watu wengi walionekana nje ya lango la kuingilia mgodini, wakisubiri taarifa za operesheni ya kutafuta waliofukiwa.

Kwa mujibu wa Teweli, baada ya mwamba huo kuporomoka, uliangukia mashine hiyo ya Jumbo na kuwabana wafanyakazi watatu.

“Jitihada za uokoaji zinaendelea katika mgodi wa Bulyanhulu,” alisema Teweli na kuongeza kwamba shughuli hizo zimekuwa zikiendelea mfululizo tangu alfajiri hadi alasiri ingawa bila mafanikio.

Alisema awali, saa 6 mchana kikosi cha waokoaji kilichokuwa chini ya ardhi kutwa nzima jana, kilisikia sauti zinazosadikiwa kuwa za wafanyakazi hao walionaswa kwenye kifusi, lakini ilipofika saa 8 mchana hazikusikika tena.

No comments: