Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma anatarajiwa kuzuru Zimbabwe hii leo ili kujaribu kutatua tofauti zilizopo kwenye serikali ya muungano kati ya chama cha ZANU PF cha Rais Robert Mugabe na MDC cha Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai.
Kama mpatanishi katika mzozo wa kisiasa nchini Zimbabwe, Rais Zuma anahitaji sana kuimarisha serikali hiyo inayolegalega, miezi kumi na tatu baada ya kuundwa kwake.
Tayari Afrika kusini ina wakimbizi milioni tatu kutoka Zimbabwe na ikiwa inajitayarisha kuandaa kinyang'anyiro cha kombe la dunia mwezi wa sita, mzozo unaoendelea kutokota nchini Zimbabwe ni jambo ambalo Rais Zuma halihitaji kabisa.
Pia juhudi za kuwapa raia wa nchi hiyo katiba mpya hazijafanikiwa kwa sasa.
Kiongozi huyo wa Afrika Kusini, anamatumaini kuwa mabadiliko ya kimsingi yataweza kufanyika, ili uchaguzi mwingine uweze kufanyika mwaka ujao.
Juhudi za Rais Zuma za hivi karibuni za kuhumiza nchi za ulaya ziondoe vikwazo dhidi ya Zimbabwe zimegonga mwamba .
No comments:
Post a Comment