ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 2, 2010

NGASSA AVUNJA SAFARI ZA CHUJI, TEGETE ULAYA



Ngassa aliyeruka juu akifunga bao katika mechi dhidi ya Sudan.
Na Saleh Ally
PAMOJA na uhamisho wa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mrisho Ngassa kuweka rekodi mpya, umesababisha tafrani kubwa ndani ya klabu hiyo hali ambayo imesababisha upitishwe uamuzi wa kutomruhusu mchezaji yoyote kujiunga na timu nyingine.

Kutokana na hali hiyo, imeelezwa Jerry Tegete na Athuman Idd ‘Chuji’ waliokuwa na ofa ya kucheza soka la kulipwa nchini Sweden sasa hawatapewa ruhusa kwa kuhofia kuzuka tafrani jingine.
Habari za uhakika kutoka Jangwani zinaeleza kuwa, kumekuwa na kutokuelewana kati ya baadhi ya viongozi na wenzao na pia upate wa mdhamini wao, Yusuf Manji ambaye amekuwa akihoji vipi Ngassa ameachiwa kwenda Azam FC kirahisi badala ya subira.
..Jerry Tegete
“Inaonekana suala hilo lingekuwa na subira, lakini mambo yameenda haraka bila kutegemewa na Ngassa ameenda Azam FC. Mdhamini amesema kulikuwa na muda wa kutosha wa kuangalia kama wanaweza kumbakisha au kumuuza Ulaya, kama yote yangeshindikana basi Azam ingekuwa ni ya mwisho. Lakini inaonekana kama lilienda kimya kimya tu,” kilieleza chanzo cha uhakika na kuongeza.
“Kuna baadhi wanamuunga mkono na wengine wanaungana na kuuzwa kwake, hali hiyo imesababisha Kocha Mkuu, Kostadin Papic amesisitiza kuangaliwa sana suala la kuuzwa mchezaji iwe kwa fedha au mkopo huku akisisitiza suala la uimara wa timu lipewe umuhimu badala ya kuuza tu wachezaji bila ya kuangalia.”

Ripoti hiyo ya Papic ya mwisho wa mwaka imesisitiza kuwa lazima kuwe na umakini ili kuepusha kuvuruga nguvu ya timu hali inayofanya safari za wachezaji wawili, Jerry Tegete anayetakiwa na Darkuld FF ya Sweden na Athuman Idd ‘Chuji’ kukwama. “Niliambiwa wakala wangu kapeleka barua ya kuniombea niende nikafanye majaribio, lakini uongozi umnatoa vipingamizi vingi,” alisema Chuji aliyetakiwa kutua Sweden juzi, huku Tegete naye akisisitiza kusikia taarifa hizo kwamba hakuna atakayeruhusiwa.
Akizungumzia suala hilo jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema hawana sababu yoyote ya kumzuia mchezaji.
“Safari hii tumekuwa wakali na tunataka uhakika. Tunataka kujua mchezaji anakwenda kwa muda gani, nani atamgharimia na itakuwaje iwapo atafuzu.
...Athuman Idd 'Chuji'
“Mfano wakala katuambia mchezaji anatakiwa kwa mkopo, hivyo tunataka kujua ni kipi kinaendelea na kila kitu kiwe wazi na ikiwezekana tuwasiliane na klabu hiyo moja kwa moja na si wakala pekee. Labda kwa ajili ya misimamo hiyo watu wanaweza kutafsiri vingine,” alifafanua Mwalusako.
Ngassa aliyekuwa amebakiza mkataba wa mwaka mmoja na Yanga, ameuzwa Azam FC na Yanga imechukua Sh milioni 58 huku ikielezwa yeye amekabidhiwa Sh milioni 40 hali iliyofanya usajili wake kuweka rekodi mpya.

Papic aliwahi kuliambia Championi kuwa Ngassa ameenda Azam FC kwa kufuata fedha tu, lakini mchezaji huyo alisisitiza hiyo ni kazi yake na anapaswa kuangalia maslahi. Gazeti hili lilikuwa ni la kwanza kuandika uamuzi wa Ngassa kuamua kuihama Yanga. Baadaye alienda kufanya mazungumzo na APR ya Rwanda hata hivyo ilishindikana na kuamua kurejea nyumbani kujiunga na Azam FC.

No comments: