ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 2, 2010

Saa 24 mbaya kwa Stars


Tuesday, 01 June 2010 23:04

Kocha marcio Maximo akiwa na wachezaji wake wakibadilishana ujuzi, wako katika maandalizi ya kuikabili timu ya Taifa ya Brazil
Jessca Nangawe
WACHEZAJI wa Taifa Stars watalazimika kucheza mechi mbili muhimu katika maisha yao ndani ya saa 24, pale watakapoikabili Amavubi nchini Rwanda na kurudi jijini kuivaa Brazil kwenye Uwanja wa Taifa.

Rwanda inayoonekana kutaka kuneemeka na mchezo wa kirafiki baina ya Taifa Stars dhidi ya Brazil ili iweze kufuzu kushiriki fainali za CHAN kwa mara ya kwanza imetangaza mchezo huo wa marudiano utachezwa siku ya Jumapili jijini Kigali huku Taifa Stars ikitakiwa kucheza pia dhidi ya Brazil Jumatatu.

Uamuzi huo wa Shirikisho la Soka la Rwanda umekuwa mtihani mkubwa kwa  TFF ambayo imeweka nguvu zake nyingi kwenye mchezo wa kirafiki wa mabingwa wa Dunia mara tano dhidi ya Stars.

Afisa Habari wa TFF, Florian Kaijage amesema kuwa Rwanda walichelewesha sana taarifa ya mechi hiyo na hata walipokuja kutoa taarifa  walisema Jumapili ambayo ni tarehe sita  kitu ambacho kimewaweka njia panda.

''Ratiba yetu tumepanga kuondoka Alhamisi kwenda Kigali, lakini mpaka sasa bado hatujamua kwani tupo kwenye mazungumzo nao kuona kama watakubali kubadilisha ratiba hiyo, lakini kama Rwanda watanga'ang'ania mechi hiyo ipo Jumapili basi huenda timu ya Taifa ikatafutiwa ndege maalumu ili tuweze kwenda kucheza mechi hiyo na kurudi siku hiyo hiyo kwa ajili ya mechi  ya Jumatatu dhidi ya Brazil,'' alisema Kaijage.

Rwanda imepania kupata ushindi kwenye mchezo huo na kufuzu kwa mara ya kwanza kwenye fainali hizo za CHAN zitazofanyika nchini Sudan 2011, pia kwa mujibu wa kanuni za CAF Rwanda ambao ndiyo wenyeji wa mechi hiyo wanaweza kuamua mechi hiyo ichezwe lini kati ya tarehe 4, 5 au 6 mwezi huu.

Viongozi wa Ferwafa, serikali na Wachezaji wa Rwanda wako kwenye ari kubwa ya kusaka ushindi kwenye mechi hiyo.

Wachezaji wake Patrick Mafisango na Haruna Niyonzima walidai kuwa Stars  isitegemee ushindi wowote.

"Hapa Rwanda ni ngumu sana kwa timu kama Tanzania kushinda kama mlishindwa Dar es Salaam ni basi, sisi tunataka kwenda fainali na ndio maana unaona maandalizi ni makubwa sana," alisema Niyonzima.

"Tanzania ina wachezaji wazuri, lakini sioni jinsi wanavyoweza kushinda hapa mbele ya watu wetu, kama kungekuwa na mechi nyingine ya kucheza ugenini wangetushinda si hapa kwetu, nakwambia tunawafunga."

Nao wachezaji wa Taifa Stars kwa nyakati tofauti waliuzungumzia mchezo huo kuwa ni mgumu, lakini wamesema watacheza kwa kujituma na kuhakikisha wanapata ushindi na kufuzu.

Katika mchezo wa awali Stars ilishindwa kuchanua makucha nyumbani kwa kukubali kulazimishwa sare ya bao 1-1.

Matokeo hayo yameiweka Stars kwenye nafasi finyu ya kufuzu kwa fainali za CHAN  mwakani nchini Sudan na endapo itafanikiwa basi itakuwa ni mara ya pili kucheza fainali hizo ambazo kwa mara ya kwanza zilifanyika nchini Ivory Coast

No comments: