ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 26, 2010

Unahitaji kudumu na mwenzi wako? Kanuni ni hii

Ndoa bora inaweza kuwa furaha kubwa ya maisha kwa wanandoa. Watu huoana kwa sababu ya mapenzi, urafiki, usiri, furaha ya ndoa na tendo lenyewe. Haya yakizingatiwa kwa muda wote, tutaepukana na ndoa za Hollywood.

Mara nyingi watu kabla ya kuoana huahidiana upendo uliotukuka na furaha. Ahadi hizo huwavutia wengi lakini ya kesho anayajua ni Mungu tu! Leo yanaweza kuwa maziwa halisi, kesho yakawa tui la nazi, ingawa weupe ni ule ule!

Kama nilivyoeleza wiki iliyopita, narudia tena kwa mkazo kwamba siku hizi ni ngumu kusimamia mapenzi yenye furaha. Na hii ni sababu tosha ya wanandoa wengi kuona talaka ni kimbilio pekee la matatizo yao.

Mwanasaikolojia Frank Gunzburg ambaye ana shahada ya uzamivu (Ph.D) katika maandishi yake kuhusu ndoa, aliyoyapa jina; “Love & Happiness Marriage and Difficulties” anasema kuwa hakuna ndoa iliyo salama ikiwa wahusika wenyewe hawataki usalama.

Aliandika: “Katika uzoefu wangu ndani ya ndoa yangu, nimejifunza jinsi ya kuwa na furaha katika hali tofauti. Hii ni kwa sababu ya ukweli kwamba hakuna ndoa iliyo kamilika lakini kuna njia za kuyafanya maisha yako ya ndoa yawe na furaha muda wote.”

Kutokana na hoja hiyo ndiyo maana nikaandaa mambo ambayo ukiyazingatia kikamilifu, yatakuwezesha kuwa na furaha ya kudumu. Unaweza kushangaa watu wanaachana, wakati wewe na mwenzako mpo kama mmeoana juzi.
MOSI: Kamwe nyote msiwe na hasira kwa wakati mmoja.

Jiulize; Wewe una hasira na yeye amekasirika, nani atambembeleza mwenzake? Inawezekana likawa gumu kutekelezeka, mimi mwenyewe nimewahi kulisoma hili kwa wataalamu waliobobea katika elimu ya saikolojia.

Nikajiuliza mwenyewe; Inawezekanaje kuepuka wapendanao kuwa na hasira kwa wakati mmoja? Inapotokea mpenzi wako hayupo sawa kwa sababu ya kitu fulani na amekasirika, kwa kawaida na wewe hilo litakuchanganya.

Anazungumza mbele yako kwa ukali, bila shaka hilo litakuudhi. Hata hivyo, inahitaji uvumilivu na uelewa kuweza kukabiliana na hali kama hiyo. Kama unampenda mwenzako, utaweza kutuliza munkari wako pale amekasirika. Kukaa kimya na kumsikiliza ni njia bora ya kuponya hisia hizo.

Sina maana ya kukaa kimya kwa mtindo wa kumdharau, la hasha! Namaanisha akizungumza wewe msikilize kwa sura inayoonesha unapokea. Akiuliza mjibu chanya. Kwa kufanya hivyo utasaidia apoe, pia baada ya hasira atafurahi kwa kumpata mpenzi sahihi.

PILI: Msifokeane, ikitokea basi iwe dharura,
kufoka kunaua mapenzi. Usimpe mwenzi wako sababu ya kukufokea. Ikitokea kuna ubishi na kila mmoja kati yenu anataka ushindi, basi tumia uungwana wako kumfanya mpenzi wako awe mshindi.

Jifunze kukubali kosa na uombe radhi. Punguza majivuno itakusaidia ndani ya ndoa. Najua ni ngumu kutekeleza lakini ni bora ujaribu.
Ni njia sahihi mno kuifanya ndoa yako kuwa imara na yenye afya. Inauma kufokewa hasa na umpendaye, ila ni hatari zaidi endapo utarudisha.

Muache afoke amalize, nawe usubiri muda muafaka wa kumueleza ni kwa kiasi gani uliumia pale alipokuwa anakukoromea. Hiyo itamsaidia kugundua kosa ili asirudie tena.
TATU: Mshukuru mwenzi wako
Jaribu kuzungumza mambo ya kupendeza kwa mpenzi wako. Kila mtu anahitaji shukrani kutoka kwa mwenzi wake. Tazama vitu chanya vya mwenzi wako kisha umueleze ni jinsi gani alivyo bora.

Kamwe usiangalie hasi. Mshukuru kwa kila anachofanikisha hata kama yeye mwenyewe atasikitika kwamba hakufanya vizuri. Mwanaume anapopongezwa hufurahi lakini furaha huongezeka pale pongezi zinapotoka kwa mkewe, hivyo hivyo kwa mwanamke dhidi ya mumewe.

NNE: Mkubali mwenzio
Tatizo kubwa kwenye migogo ya kimapenzi ni pale mmoja anapotaka kumbadilisha mwenzake. Kitu cha msingi ndani ya furaha zetu ni pale tunapohisi kuheshimiwa, kupendwa na kukubalika kwa jinsi tulivyo.

Hauwezi kujisikia vizuri pale ambapo unalazimishwa ubadilike kitabia, muonekano na kadhalika. Unapotaka kulazimisha mpenzi wako awe kama unavyotaka, utakuwa unamuumiza. Ni vema umkubali.

Ikiwa kila mmoja atajifunza kukubali na kuheshimu jinsi mpenzi wake alivyo, ndoa nyingi zitakuwa na afya. Ni ngumu kukubali muonekano au tabia za mwenzako kwa sababu unapenda awe unavyotaka lakini mtihani huu ukifaulu, inawezekana ni zawadi tosha ndani ya ndoa yako.

TANO: Wasiliana vizuri na mwenzako
Mlipokuwa wachumba mlikuwa mnawasiliana vizuri, nashangaa kwanini baada ya kuoana imekuwa tofauti! Zingatia hili kwamba kuonesha utofauti kati ya zamani na sasa ndani ya ndoa ni sumu na imezigharimu nyumba nyingi.

Mlikuwa mnatoka na kuzungumza masuala yenu, iweje leo iwe tofauti? Kukumbatiana na kupigana mabusu, inashangaza leo mnaona ni uzungu! Timiza matakwa ya ndoa yako, hivyo amka sasa na utende yale yenye faida.

SITA: Msaidie mwenzako
Uhusiano ambao unaundwa na watu wawili wanaosaidiana, mara nyingi huwa ni bora na hutawaliwa na upendo uliotukuka. Unarudi nyumbani unamkuta mwenzako anazidiwa nguvu na kabati, badala ya kumsaidia wewe unaingia na kushika hamsini zako.

Angalia matatizo ya mwenzako, yachukue kama yako halafu msaidie kuyatatua. Ikiwa yanahusu familia yake, yabebe kama vile ni ya familia yako. Kwa moyo wako wa ukarimu utaweza na hiyo itaongeza upendo ndani ya nyumba yenu.


CHANZO:GLOBAL PUBLISHERS

No comments: