ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, December 28, 2010

AG ataka Katiba iwekewa viraka

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Frederick Werema,
Waandishi Wetu 
WAKATI viongozi kadhaa wa nchini akiwamo Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, mawaziri wakuu wa zamani, Joseph Warioba na Frederick Sumaye na Jaji Mkuu Mstaafu Agostino Ramadhan wakitaka iundwe katiba mpya, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Frederick Werema, amepinga wazo hilo na kutaka katiba iliyopo iwekewe viraka zaidi.

Madai ya katiba mpya pia yamewahi kutolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, John Tendwa ambaye alisema bayana kuwa katiba mpya iandikwe mapema kabla ya mambo kuwa mabaya, akitoa mfano wa mapungufu ya katiba ya sasa kuwa ni Rais kupewa madaraka makubwa.

Jana akiwa Ikulu kwenye hafla ya kuapishwa Jaji Mkuu mpya, Mohamed Othman Chande, Werema alisema kuwa haona haja ya kuandikwa katiba mpya badala yake katiba iliyopo iwekewe viraka.

“Kuandika katiba mpya hapana, lakini kufanya marekebisho kwa kuondoa au kuongeza mambo fulani kwenye katiba ruksa,” alisema Jaji Werema.

"Suala la kubadilisha ibara zinazoonekana kutokidhi haja na kuingiza mambo mapya kwenye katiba, linakubalika na kwamba hayo yamekuwa yakifanyika," alisisitiza Jaji Werema na kutolea mfano mabadiliko ya katiba yaliyoruhusu kuingizwa kwa haki za binadamu.
 
Hata hivyo, alisema maoni ya watu yanayotolewa kuhusu katiba mpya ni sahihi kwani kila Mtanzania ana haki ya kutoa maoni yake kwa mujibu wa katiba iliyopo.

“Raha yangu ni kuona Watanzania tunajadili suala hili maana kila mtu ana haki ya kusema na ni sahihi, lakini tunatofautiana tu kama kila maoni ni sawa,” alisema Jaji Werema na kuongeza:

“Lakini si kila mtu analolisema lifuatwe. Tukisema kila mtu anachokisema tukifuate haitakuwa sawa. Kwa mfano mimi kule kwetu wafugaji nao watataka mambo ya ng’ombe wao yaingizwe kwenye katiba, na Wahaya pia wanaweza kusema tuingize kwenye katiba ndizi zao, hii si sawa;” alisisitiza Jaji Werema.

Jaji Werema alitoa wito kwa watu wote wanaojadili suala hilo kutochochea watu kuandamana na kuwataka waandishi wa habari pia kuitumia vizuri kalamu yao kuuelimisha umma.

Jaji Werema anakuwa ni kiongozi wa pili wa Serikali kupinga haja ya kuwa na katiba mpya. Kiongozi wa kwanza serikalini kupinga suala hilo alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani.

Hata hivyo, msimamo wa mwanasheria huyo wa Serikali umekuja wakati tayari Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiwa ameshaweka wazi nia ya kuyafanyia kazi madai hayo yaliyoanzishwa na Chadema na kuungwa mkono na watu wa kada mbalimbali.
Lakini wakati Jaji Werema akitoa msimamo huo, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika amesema Katiba ya Tanzania ina viraka vingi, inahitaji kuandikwa upya na viongozi wa Serikali, hawapaswi kukwepa jambo hilo.
Mnyika alisema hayo jana baada ya kupeleka barua yake kwa Katibu wa Bunge kutoa taarifa ya kusudio la kuwasilisha hoja binafsi bungeni kutaka katiba mpya huku akieleza kuwa katiba iliyopo ina kasoro 90.

Mnyika alisema kuwa katika hoja yake hiyo anayotarajia kuiwasilisha kwenye Bunge la Februari mwakani, pia ametaka katiba itakayoundwa iruhusu mgombea binafsi.

“Kutokana na kanuni za kudumu za Bunge mwaka 2004, 55(1), tunatakiwa kupeleka taarifa kuhusu  kuwasilisha taarifa  ya hoja binafsi kwa katibu na sio kupeleka hoja binafsi ya katiba,”alisema Mnyika

Alisema taarifa yake ya kusudio la kupeleka hoja binafsi bungeni aliiwasilisha jana kwa Mkurugenzi wa Idara ya taarifa za Bunge, Eliakimu Mrema ambaye alikuwa anakaimu nafasi ya Katibu wa Bunge.

Mnyika alisema baada ya kuwasilishia barua hiyo, atawashirikisha wananchi ili kupata maoni yao kabla hajaipeleka rasmi bungeni. 
Alisema  kwa sasa Chadema inakaribisha maoni kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo wasomi ,wanasiasa na wananchi wa kawaida ili watoe maoni yao kuhusu mapungufu ya katiba na wapendekeze muundo wa katiba mpya.

Alisema suala la mabadiliko la katiba nchini linamgusa kila mwananchi mwenye uelewa hivyo sio suala la kukurupuka na Chadema ilizingatia hilo ndio maana ikaamua kuwakutanisha wadau mbalimbali kupata maoni yao.
“Tutakutana na wadau wa katiba katika wiki ya kwanza ya Januari  jijini Dar es salaam katika uwanja wa wazi ambao tutautangaza baadaye ili tukusanye mawazo yao," alisema Mnyika.

Alitaja baadhi ya mapungufu yaliyomo kwenye katibaya sasa kuwa ni pamoja na suala la madaraka ra Rais ambayo kwa maoni yake, ni makubwa kuliko inavyotakia kuwa.
"Tatizo lingine la katiba yetu ni la kijamii. Katiba hii ni ya muda mrefu na kizazi kipya cha sasa hakikushiriki kuitunga hivyo ni ya kikoloni," alisema Mnyika na kuongeza:

Alisema pia sio sahihi wakurugenzi wa halmashauri kusimamia uchaguzi kwa sababu kura ni za vyama hivyo wanaopaswa kuzisimamia wanatakiwa kutokuwa mashabiki wa kisiasa.

Mnyika alisema pia kuwa katika taarifa yake hiyo amezungumzia suala la Mahakama kwamba haiko huru kwani mtendaji mkuu wa idara hiyo ambayo ni muhimili wa dola Jaji Mkuu, anateuliwa na rais.

Mkurugenzi wa idara ya taarifa za Bunge Eliakimu Mrema aliyepokea barua ya Mnyika alisema kazi ya Ofisi ya Bunge ni kupokea taarifa na kuzifanyia kazi hivyo taarifa hiyo imefika.
Katika hatua nyingine, Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba, amesema kuwa suala sio kuifanyia marekebisho katiba iliyopo bali kutunga katiba nyingine.

Mukoba aliliambia gazeti hili jana kuwa katiba ya sasa ni ya kikoloni kutokana na kumpa Rais madaraka makubwa hali ambayo inasababisha kuzorotesha maendeleo ya nchi
“Mfano kitendo cha viongozi kuchukua fedha za EPA na rais kuamua kuwasamehe na kusema watarudisha taratibu ni sababu ya katiba kumpa madaraka makubwa; yaani kuwa juu ya sheria maana rais hatakiwi kuwa na mamlaka ya kuwasamehe wezi,”alisema Mukoba.

Alisema kuwa katiba mpya inayohitajika sasa ni ile ambayo haimpi Rais madaraka makubwa kama hayo na kwamba kitendo cha rais kuwa juu ya sheria ni chanzo cha viongozi kuwa na utovu wa nidhamu.

Mukoba alisema kuwa hata majaji hawatakiwi kuteulewa na Rais badala yake wangethibitishwa na Bunge kama ilivyo kwa Waziri Mkuu.

“Ukweli ni kwamba viongozi wote wanaoteuliwa na Rais wanafanya kazi kwa nidhamu ya woga na kutaka kulinda maslahi yao maana wakisema ukweli wanaweza kupoteza kibarua chao,”alisema Mukoba.

Habari hii imeandaliwa na James Magai, Hussein Issa na Gedius Rwiza

1 comment:

Anonymous said...

ili kuwepo haki na demokrasia ya kweli ni lazima maoni/matakwa ya wengi yatimizwe.(majority rule) mwelekeo wa nchi nzima hauwezi kuamuliwa namtu mmoja au kundi la watu wachache(dictatoship). Tanzania ni nchi ya demokrasia sio nchi ya kidikteta,huyu mwanasheria mbuzi arudishwe kwao alikotoka,awaachie wananchi wa Tanzania waamue uelekeo wa nchi yao.....Dictator Id Amini alisha kufa miaka mingi..hatuhitaji udikteta mpya !!tunataka tuamue woooote !!