
Jana (Jumatatu) ilikuwa ni Siku ya Wapendanao duniani maarufu kama Valentine’s Day. Ingekuwa wapenzi wote wameadhimisha kwa furaha nisingekuwa na haja ya kuandika makala haya lakini kwa sababu wengine walikerwa na wapenzi wao kwa kutopewa kipaumbele kwenye sherehe hiyo nimeona nifundishe somo la haki na wajibu katika mapenzi.
Msomaji wangu, maisha ya kimapenzi yana nguzo kuu mbili ambazo ni HAKI kwa mantiki ya jambo analostahili mtu kulipata na WAJIBU kama suala la lazima kwa mwanadamu kulitimiza.
Nikisema hivi nina maana kwamba Siku ya Wapendanao tuliyoiadhimisha ilikuwa na mambo makuu mawili, yaani haki na wajibu. Lakini pengine jambo muhimu la kulitupia macho ni jinsi gani wapenzi wanaweza kujenga nguzo hizi kwa wakati mmoja.
Kanuni za kitaalamu zinaelekeza kwamba WAJIBU ni kitu cha kwanza kufanywa na mwanadamu kabla ya HAKI kuchukua nafasi. Popote duniani ukitaka kupata haki lazima wewe mwenyewe uwajibike.
Kwa mfano unapotaka haki ya kupewa elimu unalazimika kwenda darasani, huwezi kukaa tu nyumbani ukisubiri mwalimu aje akufundishe. Lazima uwajibike kwenda shule na utii sheria.
Katika hali ya kawaida, wajibu ni jambo gumu sana kwa sababu huambatana na gharama, ndiyo maana wengi wetu tunakimbilia kudai haki yenye faida.
Ukiangalia kwa undani, mapenzi ya siku hizi yamejaa hitaji la haki lisilozingatia wajibu. “Mimi kama mke nina haki ya kupewa mavazi na kuhudumiwa.” Lakini ukimuuliza mwanamke huyo kama amewajibika kwa mumewe linakuwa swali gumu.
Hebu tujiulize sisi kama wapenzi, tulipokuwa tunadai haki ya kushirikishwa kwenye Siku ya Wapendanao, tulipotaka kununuliwa kadi, nguo, kutolewa ‘out’ na kuandaliwa sherehe, ni wajibu gani tuliufanya kwa wenzetu?
Je, tuliwajibika katika heshima, upendo, kujali na kujitolea au tulikaa kimya tukisubiri tutendewe haki isiyokuwa na wajibu mpaka leo tunalaumu?
Hata kama mtu ulikuwa huna pesa, ulikuwa na sababu ya kukumbusha umuhimu wa kuwa pamoja siku hiyo. Ulikuwa na wajibu wa kujitoa kwa hili na lile hata kwa kauli safi: “Mpenzi hali yangu kifedha si nzuri lakini naomba usiitumie vibaya Valentine Day, tuwe pamoja, saa nne nitakupitia kwako.”
Wajibu huu ungetosha kukupa haki ya kupewa nafasi kusherekea pamoja siku hiyo muhimu lakini ulipokuwa mkimya, uliyejaa ukorofi na vurugu za kutaka haki ya kununuliwa nguo na kadi au kupewa fedha za kutoka ‘out’ ndivyo ulivyosababisha tatizo la kutopewa haki.
Mwisho nawaomba wapenzi wote wazingatie somo hili la wajibu na haki kwenye mapenzi. Ukiwa kama mwanaume usikimbilie kudai haki tu, wajibika kama kiongozi wa familia.
Jitolee, fundisha na tumia busara katika kutatua migogoro. Usiwe mtu wa kudai chakula kwa nguvu wakati hujaacha fedha wala kudai heshima ya mume wakati wewe mwenyewe hujiheshimu.
HAKI NA WAJIBU LAZIMA VIENDE .PAMOJA
No comments:
Post a Comment