MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, leo amemtaka Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Balozi Hamisi Kagasheki,afute kauli yake aliyoitoa bungeni kuwa Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Conchesta Rwamlaza,anatoa siasa za jimboni kuleta bungeni.
Zitto amesema bungeni mjini Dodoma kuwa, hairuhusiwi wabunge kushutumiana ndani ya Bunge.
Kwa mujibu wa Mbunge huyo, Rwamlaza na balozi Kagasheki wanafanya kazi pamoja kwa kuwa kiongozi huyo wa Serikali ni Mbunge wa Kigoma mjini hivyo afute kauli yake.
Zitto amesema, alichokisema Rwamlaza si mambo ya siasa, na kwamba, anamheshimu sana Balozi Kagasheki.
Spika wa Bunge, Anne Makinda, amesema, Zitto yupo sahihi, na kwamba hakufahamu kama Kagasheki anajibu kwa kutumia nafasi ya ubunge na si wadhifa wake wa unaibu waziri.
Makinda amesema, kama angejua Kagasheki angeyasema hayo asingemruhusu lakini amesema, majibu ya kiongozi huyo ni sahihi.
Balozi Kagasheki alimshutumu Rwamlaza kwa kusema kuwa, suala la uharibifu uliotokana na ulipuaji wa miamba kwa ajili hya upanuzi wa uwanja wa ndege wa Bukoba na fidia kwa waathirika ni siasa zaidi na kwamba si vizuri kupeleka siasa bungeni.
Wakati akijibu swali la msingi la Mbunge huyo, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Athumani Mfutakamba alisema, Serikali ilifanya tathimini kuhusu upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Bukoba ikiwa ni pamoja na kufahamu athari za upanuzi wa uwanja huo kwa mazingira na kupata kibali cha upanuzi kutoka Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment