MTUNZA bustani mkazi wa Mbezi Juu Mtoni, Dar es Salaam, Shabani Kihundo (30), amekutwa amekufa chumbani kwake baada ya kunywa sumu kutokana na kutoelewana na mkewe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema Kihundo alikutwa amekufa juzi saa 7.00 mchana, huko Mbezi huku akiwa amelala kifudifudi.
Ilidaiwa kuwa katika eneo hilo, chini ya kitanda kulikutwa matapishi na pembeni yake palikutwa na chupa yenye majimaji inayoonesha mabaki ya sumu aliyokunywa ambayo haijafahamika ni ya aina gani.
Kwa mujibu wa Kamanda Kenyela, Kihundo aliacha ujumbe uliooneshwa kuwa kati yake na mkewe kulikuwa na ugomvi.
Ujumbe huo ulisomeka, “Nimejiua kutokana na kutoelewana na mke wangu na malengo yake yametimia/ yamekamilika, nimeona nimuachie dunia kwa sababu nimeamua kutuliza nafsi yangu, nimeshindwa, nilimpenda nimeona sina umuhimu wa kuishi tena duniani.”
“Ahsante kwa kuninyima haki yangu, nimekuachia nyumba ukiamua kukaa ukae, ukiamua kuuza hiyo ni haki yako sio mimi, Samwel ananidai Sh 28,000.
“Pia mimi ni mwanachama wa NSSF na kadi yangu anayo mke wangu, atachukua Sh milioni moja ili zimsaidie kwa sababu atakuwa na shida na maisha magumu, baiskeli apewe mdogo wake mke wangu pamoja na viatu, nguo na vitu vingine. Asante wako wa moyoni.”
Maiti imehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala kwa uchunguzi zaidi huku polisi wakiendelea na upelelezi na hakuna mtu anayeshikiliwa kwa kuhusishwa na tukio hilo.
CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment