Advertisements

Tuesday, March 29, 2011

Diwani adaiwa kusimamia baba yake auawe

DIWANI wa Kata ya Ipinda wilayani Kyela, Hunter Mwakatuma, anadaiwa ‘kusimamia’ mauaji ya baba yake mzazi kwa madai ya baba huyo amehusika katika kifo cha mwanawe ambaye ni mdogo wa diwani huyo. 

Baba huyo, Albert Mwakatuma, ambaye umri wake haujafahamika na mkazi wa Kijiji cha Mabunga katika kata hiyo, aliuawa Jumatano iliyopita kwa kupigwa mawe na wakazi wa kijiji hicho mara baada ya maziko ya mwanawe, Mawazo Mwakatuma. 


Kabla ya mauaji hayo ya kinyama, mtoto wa mzee huyo, Macklini, aliugua ghafla na kufariki dunia na baba huyo kutuhumiwa kuwa mchawi aliyemroga kijana huyo. 

Wakati tuhuma hizo zikiendelea kusambaa dhidi ya baba huyo, baada ya maziko ya kijana huyo waombolezaji walimpiga mawe na marungu baba huyo na kumuua mbele ya diwani huyo na baadhi ya askari wa Polisi. 

Inadaiwa kabla na baada ya kifo hicho, diwani huyo aliagiza polisi wasikamate mtu yeyote, kwa madai kuwa tukio hilo la mauaji ni la kiukoo na hivyo litamalizwa kiukoo. 

Hata hivyo, taarifa za mauaji hayo zilimfikia Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile, aliyekuwa ziarani Kyela ambaye alimwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi, kutoa maelezo ya kwa nini hajachukua hatua dhidi ya wauaji. 

Mbali na kutoa maelezo hayo, Mwakipesile aliagiza polisi Kyela kumkamata diwani huyo na polisi waliokuwa eneo la tukio kwa kushindwa kuzuia mauaji hayo, jambo linaloonesha walishiriki kutetea uhalifu. 

“Mpaka sasa nasikia wamekamatwa watu wanane tangu nitoe agizo jana lakini kwa nini mpaka RC (Mkuu wa Mkoa) aagize ndipo hatua zichukuliwe na kwa nini kati ya waliokamatwa hawamo askari walioshindwa kutetea uhai wa marehemu au kuwakamata wauaji? 

Kwa nini mpaka leo diwani hajakamatwa kwa kuzuia kukamatwa kwa wahalifu? Eti ni masuala ya kiukoo tutayamaliza kiukoo! Mtu anauawa kinyama kwa imani za kijinga wewe unasema ni masuala ya kiukoo! Sasa nataka wale wote waliokuwapo akiwamo diwani na askari, wakamatwe wawekwe ndani,” aliagiza Mwakipesile. 

Alisema, Serikali haiwezi kuvumilia vitendo vya mauaji ya kinyama kama hivyo vinavyosababishwa na imani za kishirikina, zisizo na ushahidi wowote. 

Mwakipesile alisema hali kama hiyo ikiachiwa iendelee, watu wanaweza kutumia mwanya huo kutimiza azma zao za kutopenda maendeleo ya wenzao na kuwazushia kashfa za kishirikina. 

Alitoa mwito kwa wakazi wilayani hapa kuachana na imani hizo badala yake watambue kuwa maendeleo ya mtu yanatokana na kujituma kwa mhusika katika shughuli zake zinazolenga kutekeleza mipango aliyojiwekea na si vinginevyo. 

Matukio ya wananchi kujichukulia sheria mikononi na kupiga hadi kuua raia kwa tuhuma mbalimbali hasa za wizi na uchawi, yamekithiri mkoani hapa huku wengi kati ya watuhumiwa wa matukio hayo wakiwa hawachukuliwi hatua na Polisi.


CHANZO:HABARI LEO

No comments: