.jpg)
Wakati hofu ya kuhujumiwa ikiifanya Simba ichelewe kwenda nchini Kongo, kocha wa klabu hiyo ya Msimbazi, Patrick Phiri amewaweka roho juu wachezaji wake baada ya kuamua kwamba hatataja hadi baada ya mazoezi ya kesho asubuhi majina ya nyota watakaoenda kuwakabili mabingwa wa Afrika, TP Mazembe katika mechi yao ya awali ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika mjini Lubumbashi.
Ili kukwepa vitendo vyovyote vya kuwaondoa wachezaji wa Simba katika hali ya mchezo, uongozi wa Simba umepanga kuipeleka timu hiyo siku moja kabla ya mchezo huo.
Akizungumza na NIPASHE, Afisa Habari wa klabu ya Simba Cliford Ndimbo alisema kuwa timu hiyo huenda ikaondoka nchini Jumamosi ikiwa ni siku moja kabla ya mchezo huo.
Alisema kikosi cha timu hiyo kitaondoka kwa ndege ya kukodi ambayo pia itawasubiri kuwarudisha nchini mara baada ya mchezo huo.
"Kikosi chetu huenda kikaondoka Jumamosi kwa ndege kuelekea Lubumbashi kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya TP Mazembe," alisema Ndimbo.
Alisema kuwa kikosi hicho kitaondoka na wachezaji 20 na kwamba wachezaji walio majeruhi mlinzi wa kati Joseph Owino, kiungo Uhuru Seleman na Abulhalim Humoud hawatakwenda.
Kocha msaidizi wa Simba, Amri Said alisema kuwa timu hiyo inaondoka mjini Arusha leo kuja Dar es Salaam kwa ajili ya safari ya Lubumbashi.
"Tunategemea kuondoka huku kesho (leo) kuja Dar es Salaam ambapo kati ya Ijumaa jioni na Jumamosi tutaanza safari kutoka Dar kwenda Lubumbashi," alisema Saidi.
Alisema kuwa wachezaji wote wa timu hiyo wapo kwenye morali ya juu na wanaamini watafanya vizuri kwenye mchezo huo wa ugenini.
Aliongeza kuwa kufikia jana hakuna mchezaji mwingine aliye majeruhi ukiondoa wachezaji watatu waliotajwa na msemaji wa timu hiyo.
Baada ya mchezo huo wa Jumapili, Simba watarudiana tena na mabingwa hao watetezi mara mbili mfululizo wa Afrika wiki mbili baadaye jijini Dar es Salaam.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment