
Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia siha njema na pia kwa kunipa mwangaza wa kuandika yale ambayo yamekuwa yakiwasaidia katika maisha yenu ya kimapenzi.
Wiki iliyopita utakumbuka nilianza kuzungumzia mambo wanayoyatarajia wanaume wengi kutoka kwa wanawake na leo nitamalizia sehemu iliyobaki kisha tuweze kuendelea na mada nyingine.
Niliishia kuzungumzia ishu ya kuaminiwa. Wanaume wengi hasa wale wanaojiheshimu na kuujali uhusiano wao, hukasirika sana kuona wapenzi wao hawawaamini.
Wengi wanapenda kuaminiwa na hata pale ambapo wataonekana ‘hawajatulia’, wanatarajia kuelezwa huku ushahidi ukiwepo. Kwa maana hiyo ukiwa ni mtu wa kumchukulia mume au mpenzi wako kwamba anakusaliti wakati huna ushahidi wowote, unamkwaza.
Ukiona dalili fulani za kwamba anakuzunguka, fuatilia ili kujua ukweli kuliko kuanza kueleza namna usivyomuamini bila kuwa na vielelezo.
Kubembelezwa
Wanawake wengi wamekuwa wakijisahau na kudhani wao tu ndiyo wenye haki ya kubembelezwa lakini wanaume hawana haki hiyo.
Kama ulikuwa hujui, wanaume wengi wanapenda kuchukuliwa kama watoto. Wanapenda kubembelezwa na kudekezwa kimtindo kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku.
’No’ ubishi
Iwe ni mwanaume au mwanamke, kila mmoja ana haki ya kusikilizwa lakini kiukweli wanaume wanapenda kusikilizwa zaidi na hawapendi kubishiwa katika yale ambayo wanaamini yana ukweli.
Kwa maana hiyo basi, epuka tabia ya ubishi kwa mpenzi wako, hata kama analokuambia halikuingii akilini, msikilize kwanza kisha uangalie njia ‘laini’ ya kumfikishia ujumbe kwamba anachokuambia si sahihi.
Kujenga familia pamoja
Ni asilimia ndogo sana ya wanaume wanaoingia kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa lengo la kusogeza siku, wengi wanataka wapenzi wa kujenga nao familia.
Je, wewe unaonesha kwamba uko tayari kumalizia siku zako zilizobaki hapa ulimwenguni na yeye au unaonesha upo kimasilahi zaidi? Bila kukuficha ni kwamba, mwanaume akishaona uko kimasilahi zaidi, atakuacha siku si nyingi.
Kwa kumalizia naomba niseme maneno yafuatayo kwenu ninyi wanawake mliobahatika kusoma makala haya.
Kimaumbile wanaume wanapenda kuona wanasikilizwa na wake zao au wapenzi wao na hawakawii kubadilika wanapokwazwa.
Pamoja na kwamba nanyi mna sauti, lakini wanaume ni watu wa kuwasoma kwanza na kuwaendea taratibu kuliko kuwapandishia na kuonesha kushindina nao. Kama kweli unampenda basi muoneshe unamheshimu, hapo utampata!
Wanaume hupenda wanawake wasafi, wakarimu, wacheshi na wasio na kiburi wala nongwa zisizokuwa na maana. Hivyo basi jitahidi katika hayo ili ukonge moyo wa mpenzi wako na kamwe hatakusaliti.
Lakini huwa nasikitishwa sana na hizi zama za usawa ambazo zinachochea migogoro mingi katika uhusiano wa kimapenzi. Kwa mfano, hivi sasa mwanamke kumtii mumewe kunachukuliwa ni kama utumwa!
Nawahakikishia, kwa ninavyofahamu hisia za wanaume walio wengi, hali hii ikiendelea sidhani kama kutakuja kuwa na mapenzi imara, sana sana mapenzi yatageuka kuwa uwanja wa mapambano na ushindani siku zote.
Nawaomba akina dada, pamoja na elimu mliyonayo, jitahidini kujilazimisha kuwaheshimu waume zenu kwani kamwe hamtapungukiwa na kitu bali mtajihakikishia mapenzi yenye utulivu na amani siku zote za maisha yenu!
Naomba niishie hapo kwa leo, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine kali zaidi.
No comments:
Post a Comment