Mkazi wa Muungano Wilaya ya Chamwino mkoani hapa, Job Mhanga (40), ameuawa kwa kuchomwa visu sehemu mbalimbali za mwili baada ya kufamaniwa akifanya mapenzi na mke wa mtu.
Aidha, Rehema Mathayo (36), amejeruhiwa katika tukio hilo baada ya kuchomwa visu ubavuni na mumewe, Joseph Chidoho (40).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Zelothe Stephen, alisema tukio hilo lilitokea saa 9.00 usiku wa kuamkia jana katika kijiji cha Muungano, wilayani humo.
Akielezea tukio hilo, Kamanda Stephen, alisema Rehema aliaga kwa mumewe kuwa anakwenda nyumbani kwao kusherehekea sikukuu ya Pasaka. Hata hivyo, alisema mumewe (Joseph), alimfuatilia na kumkuta akiwa na mwanamume mwingine (Job), nyumbani kwao katika kijiji hicho na kuzua vurugu kubwa.
“Joseph aliyekuwa akimfuatilia mkewe alimkuta akiwa na mwanaume mwingine na kumchoma visu sehemu mbalimbali na pia kumjeruhi mkewe kwa kumchoma visu ubavuni,” alisema Kamanda Stephen.
Alisema Rehema amelazwa katika Hospitali ya Mvumi Mission akipatiwa matibabu wakati Job alifariki dunia eneo la tukio.
Hata hivyo, alisema habari nyingine zinasema kuwa mwanamke huyo alikuwa na ugomvi na mumewe hali ambayo ilimfanya kuondoka na kurudi nyumbani kwao.
Alisema shauri hilo lilifikishwa kwa mwenyeti wa kijiji ambapo Joseph alikuwa akimsihi mkewe kurejea nyumbani. Kamanda Stephen alisema mtuhumiwa huyo alitoroka baada ya tukio na kwamba juhudi za kumsaka zinaendelea ili afikishwe katika vyombo vya sheria.
Wakati huo huo, mtu mmoja anayesadikiwa kuwa kibaka, Mohamed Juma (30), ameuawa kwa kupigwa na wananchi wakati akijaribu kuiba.
Kamanda Stephen alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 3:45 asubuhi katika kata ya Ng’ong’ona, karibu na Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).
Alisema maofisa wa Kampuni ya Ujenzi ya Beijing wanaojenga katika eneo, waliona mtu aliyekuwa akiingia eneo hilo kwa nia ya kuiba.
Alisema maofisa hao walipiga kelele za kuomba msaada kutoka kwa wananchi wanaoishi jirani na eneo hilo ambao walifika na kuanza kumshambulia.
Alisema mtu huyo alifariki dunia muda mfupi kabla ya kufikishwa hospitali.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment