Kesi tatu kubwa zatakiwa kortini
Lipumba aasa bila hivyo ni kazi bure
Lipumba aasa bila hivyo ni kazi bure.jpg)
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema watuhumiwa wa ufisadi wanapaswa kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili na si kupewa siku 90 kujiuzulu ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) tu.
Profesa Lipumba alisema hayo zikiwa zimepita siku 18 tangu dhana ya CCM ya ‘kujivua gamba’ ianze kutekelezwa kwa Sekretarieti na Kamati Kuu (CC) kujiuzulu na kuteuliwa sekretarieti na CC mpya, baada ya vikao vya CC na NEC ya chama hicho, vilivyofanyika Aprili 9-11, mwaka huu mjini Dodoma.
Uamuzi huo ulielezwa na viongozi kadha wa chama tawala kuwa una lengo la kurejea katika maadili kwa kuwaondoa viongozi wanaokiletea sifa mbaya chama hicho ili kurejesha imani ya wanachama na wananchi kwa ujumla.
“Kama kweli CCM ina dhamira ya kupambana na rushwa, serikali iwafungulie mashtaka wenye tuhuma za rushwa,” alisema Profesa Lipumba jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Profesa Lipumba alisema tuhuma za ufisadi dhidi ya viongozi kadhaa wa CCM ni nyingi na za kweli.
UFISADI WA RADA BADO
Alitoa mfano jinsi serikali ya Tanzania ilivyonunua rada ya bei juu kutoka kampuni ya BAE ya Uingereza kwa dola za Marekani milioni 40 (Sh. bilioni 60) wakati wataalamu wa kimataifa wa mambo ya anga wa ICAO walishauri rada inayokidhi mahitaji ni dola za Marekani milioni 5 (Sh. bilioni 7.5).
Lipumba alisema baada ya ununuzi kufanyika, Taasisi Inayoshughulikia Makosa Makubwa ya Jinai ya Uingereza (SFO), iligundua kuwa mfanyabiashara, Saileth Vithlani, alilipwa na BAE dola za Marekani milioni 12.4 (Sh. bilioni 18.6) asilimia 30 ya bei ya rada ili kuishawishi serikali ya Tanzania ikubali kununua rada hiyo.
Alisema baadaye makachero wa SFO waligundua kuwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya CCM, ambaye ni Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, ana akaunti yenye zaidi ya dola za Marekani milioni moja (Sh. bilioni 1.2) katika kisiwa cha Jersey, nchini Uingereza.
“Barua ya SFO kwenda kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilileza kuwa Saileth Vithlan alihamisha fedha zaidi ya dola za Marekani milioni moja kutoka kwenye akaunti zake na kupeleka kwenye akaunti zinazomilikiwa na Chenge,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema makachero wa SFO waliifahamisha serikali ya Tanzania kuhusu akaunti za Vithlani na uhusiano wake na BAE, pia walimhoji Vithlani hapa hapa nchini mbele ya maafisa wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru).
Hata hivyo, alisema Vithlani aliruhusiwa kuondoka nchini bila kubughudhiwa na baada ya kuwa ameondoka, ndipo Takukuru ikajikakamua kupeleka kesi mahakamani Novemba 2007 na kutoa wito kuwa Vithlani anatafutwa.
Hata hivyo, Profesa Lipumba alisema hadi sasa hakuna ofisa yoyote wa serikali aliyeshtakiwa pamoja na Vithlani.
“Suala la kujiuliza ni kwanini Vithlani hakukamatwa na kuwekwa ndani kuisaidia Takukuru kuwanasa walioshirikiana naye baada ya serikali kupata taarifa ya akaunti zake toka SFO?” alihoji.
Profesa Lipumba alisema kumalizika kwa kesi ya rada nchini Uingereza, hakufuti makosa ya rushwa yaliyofanywa na Vithlani nchini na wale waliopokea fedha kutoka kwake.
Alisema iwapo kweli CCM ina nia ya kupambana na rushwa, serikali inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete itumie ushahidi walioletewa na SFO kuwafikisha mahakamani wote waliopokea fedha kwenye akaunti zao kutoka kwa Vithlan.
Mwenyekiti huyo wa CUF, alisema pamoja na hivyo, serikali imeshindwa kuziomba paundi milioni 29.5 zilizotolewa kama fidia kwa Watanzania kwa kuuziwa rada ya bei ya juu.
KAGODA KINARA UCHOTAJI EPA
Aidha, Profesa Lipumba alisema kuwa kampuni ya Kagoda Agriculture Limited ndiyo iliyoasisi uchotaji wa dola za Marekani milioni 113 kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (Epa) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Profesa Lipumba alisema Kagoda ilifanya wizi wa wazi wa kughushi nyaraka na kufungua milango kwa wengine kwenda kuchota fedha hizo.
Hata hivyo, alisema hadi sasa wamiliki wake wa kweli hawajatajwa na serikali wala kufikishwa mahakamani, pia uhakiki wa fedha za Epa zilizorudishwa serikalini haujafanyika na kuwekwa wazi.
RICHMOND/DOWANS
Pia alisema sakata la kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond na Dowans, limesababisha hasara kubwa kwa Watanzania na serikali.
Alisema sheria ya Takukuru inaeleza wazi kuwa kitendo cha kusababisha hasara kubwa kwa serikali ni kosa la rushwa.
Hata hivyo, alisema waliohusika kuipa Richmond mkataba wa kufua umeme, hawajafikishwa mahakamani kwa kuiletea serikali hasara kubwa.
Alisema hakuna ofisa wa serikali ameshitakiwa kwa kashfa ya Richmond/Dowans.
Profesa Lipumba alisema serikali ya CCM imeshindwa kupambana na rushwa kwa sababu vigogo wengi wamehusika au kunufaika na ufisadi huo.
AMVAA MKAPA
Alisema matukio ya rushwa na ufisadi mkubwa nchini yalitokea katika kipindi cha uongozi wa Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.
Profesa Lipumba alisema yeye binafsi (Mkapa), alivunja sheria na kanuni za maadili ya uongozi kwa kutumia Ikulu kuanzisha kampuni na kukopa dola za Marekani 500,000 benki, ambazo zililipwa ndani ya mwaka mmoja.
Alisema pia alibinafsisha mgodi wa makaa ya mawe Kiwira kwa kampuni ya familia na rafiki zake kwa bei poa ya Sh. milioni 700, lakini wakalipa Sh. milioni 70 tu, huku bei ya soko ya mgodi huo ikikadiriwa kuwa Sh. bilioni nne.
“Rais Mkapa alikuwa jasiri alipoingia madarakani mwaka 1995 na alitangaza mali zake, lakini baada ya kumaliza kipindi cha miaka 10 cha urais wake ameshindwa kuwaeleza Watanzania ana kiasi gani cha mali,” alisema Profesa Lipumba.
Aliongeza: “Mama wa ufisadi wote ulifanyika mwisoni mwa kipindi cha pili cha Rais Mkapa na kilihusu kutumia Epa kuibia serikali Sh. bilioni 130… Fedha za serikali zilizoibwa kutoka BoT mwaka 2005 inawezekana kuwa ni nyingi zaidi ya Sh. bilioni 130 zilizogunduliwa baada ya ukaguzi wa akaunti ya Epa.”
Hata hivyo, alisema serikali haiwezi kufanya hivyo kwa vile ufisadi unawagusa vigogo wengi wa CCM.
“Huenda hata hao wanaotishiwa kufukuzwa baada ya siku 90 wasiguswe kabisa hasa watakapotishia kufichua siri nyingi za walionufaika na ufisadi wao. CCM haina uwezo wa kupambana na rushwa, inachoweza kufanya ni usanii dhidi ya rushwa,” alisema Profesa Lipumba.
Alitaka viongozi na watendaji serikalini waliojilimbikizia mali isiyoelezeka kwa vipato vyao halali wafikishwe mahakamani kwa mujibu wa sheria, pia Takukuru ipewe uongozi mpya ulio makini na jasiri wa kupambana na rushwa.
Alisema CUF itaunga mkono hata mtu asiye kuwa raia kama vile John Githongo aliyeonyesha uwezo mkubwa wa kupambana na rushwa Kenya, kupewa kazi ya kuongoza au kuishauri Takukuru.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment