Harakati za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kulirejesha Jimbo la Mbeya Mjini kutoka mikononi mwa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) zimeanza rasmi, baada ya Sekretarieti ya Chama hicho wilaya ya Mbeya Mjini kuitisha kikao cha pamoja na Sekretarieti ya Mkoa wa Mbeya kwa ajili ya kupanga mikakati ya kujivua gamba la kiutendaji.
Jimbo la Mbeya Mjini ambalo kwa muda mrefu lilikuwa likiongozwa na mbunge wa CCM, katika uchaguzi uliopita liliangukia mikononi mwa Chadema, baada ya aliyekuwa mgombea wa kiti hicho kupitia CCM, Benson Mpesya, kubwagwa kwa kura nyingi na Mbunge wa sasa, Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina la Mr. II Sugu wa Chadema.
Akizungumza na NIPASHE mjini hapa jana, Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Mbeya Mjini, Athanas Kapunga, alisema kikao hicho kitafanyika kesho.
“Jumatano (kesho) tutakuwa na kikao cha Sekretarieti ya Wilaya kwa pamoja na Sekretarieti ya Mkoa kwa ajili ya kupanga mikakati yetu ya kiutendaji kwa ajili ya kukijenga chama chetu hapa Mbeya Mjini, baada ya kikao hicho sasa tutaanza kushuka katika ngazi za chini kuimarisha chama," alisema Kapunga.
Kapunga ambaye pia ni Meya wa Jiji la Mbeya alisema kikao chicho kitafanyika katika makao makuu ya Chama Mkoa wa Mbeya na kuwa tayari wajumbe wote wa Sekretarieti ya wilaya ya Mbeya Mjini na Mkoa ameshajulishwa kuhudhuria.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment