ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 27, 2011

Azam yamuweka sokoni Ngassa

Uongozi wa timu ya soka ya Azam FC ya jijini Dar es Salaam umesema kuwa uko tayari kumuuza mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu uliomalizika, Mrisho Ngassa lakini ukitoa angalizo kuwa klabu yoyote inayomtaka ijiandae kuvunja 'benki' ili kumtwaa.
Ngassa amekuwa akitajwa na baadhi ya wadau wa Yanga kwamba huenda akarejea katika klabu yake hiyo ya zamani na kwamba tayari Kamati ya Usajili ya Wanajangwani inatarajia kufanya harambee maalumu kusaka fedha zaidi za usajili.

Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa Azam, Idrissa Nassor, alisema kwamba wao walimsajili Ngassa kwa gharama kubwa na kwamba ni miongoni mwa nyota wanaotegemewa kikosini, hivyo klabu inayomtaka ni lazima ijiandae kulipa dau kubwa ili kumtoa mikononi mwao.
Nassor alisema aliongeza kuwa mbali na mchezaji huyo kuwa ghali, vilevile yuko katika mipango yao ya kuipa mafanikio Azam na kwa sababu hiyo, atakayetaka kumuhamisha itabidi awalipe fedha zaidi ya zile ambazo walimnunulia wakati akitokea Yanga.
"Ni lazima timu itakayomtaka ijiandae kulipa gharama kubwa, sisi pia alitugharimu kiasi kikubwa cha pesa wakati tunamchukua Yanga," Nassor aliongeza.
Hata hivyo, kiongozi huyo alisema kuwa bado hawajapokea maombi rasmi kutoka kwa klabu yoyote nchini na nje ya nchi na kwamba, endapo itatokea watakuwa tayari kukaa mezani na kujadiliana.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Seif Mohamed, alisema kwamba klabu yake haina nia ya kumsajili nyota huyo anayechezea timu za taifa (vijana chini ya umri wa miaka 23 na Taifa Stars).
Alisema kuwa hivi sasa wako katika mipango ya kufanyia kazi mapendekezo ya kocha wao Sam Timbe, ili wafanye vizuri katika msimu ujao na mashindano ya Klabu Bingwa Afrika mwakani.
Usajili wa Ngassa mwaka jana ulivunja rekodi ya uhamisho nchini kwani ilidaiwa kuwa gharama za jumla za kumtoa Jangwani zilifikia Sh milioni 98, Ngassa mwenyewe akidaiwa kulipwa Sh milioni 40 na kiasi kilichobaki kikitua Yanga.
Hata hivyo, mshambuliaji Mbwana Samatta ameweka rekodi mpya nchini baada ya kuuzwa kwa klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa gharamza za jumla za dola za Marekani 150,000, ambazo ni sawa na Sh milioni 224, Samatta mwenyewe akilipwa dola 50,000 (Sh milioni 75) na nyingine zikilipwa kwa Simba.
CHANZO: NIPASHE

No comments: