Mbunge wa Kahama, James Lembeli, ameshauri wimbi la kujivua gamba ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) liendelee hadi ngazi ya mkoa, wilaya, kata na matawi ambako amedai kumejaa mawakala wa mafisadi.
Alisema kamati ya siasa ya mkoa wa Shinganga inayoongozwa na Hamisi Mgeja, nayo inapaswa kujivua gamba kwani imeshindwa kutimiza wajibu wake.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa, Lembeli alisema kuwa watu hao wamechangia nchi kuingia katika mtafaruku mkubwa na kusababisha wananchi wakose imani na chama na serikali yao.
“Mwenye macho haambiwi tazama, kila mmoja anafahamu huku mikoani ndiko kwenye chanzo cha ufisadi na kwa upande wa Shinyanga imefikia mpaka wananchi wanakipa adhabu Chama Cha Mapinduzi kutokana na makosa ya viongozi walioko katika kamati ya Siasa,” alifafanua.
Alisema ushahidi uko wazi kwani mkoa wa Shinyanga ndio ulikuwa ngome kuu ya CCM, lakini hivi sasa umegeuka kimbilio la vyama vya upinzani na vimefanikiwa kupata mavuno makubwa katika nafasi za ubunge.
Alieleza kuwa mkoa huo wenye utajiri mkubwa wa madini ya dhahabu, mifugo, kilimo cha pamba na mbunga, umepoteza majimbo matano kati ya 11.
Alitaja majimbo hayo kuwa ni pamoja Bariadi Mashariki, Maswa mashariki, Maswa Magharibi, Bukombe na Meatu.
“Kupotea kwa majimbo hayo kunatokana na ufisadi uliopo ndani ya baadhi ya viongozi wa CCM katika mkoa huo na ili kurekebisha hali hii ni lazima viongozi hao wajivue gamba kwani wanajali zaidi maslahi binafsi, rushwa, upendeleo na hawana uzalendo,” alisisitiza.
Aidha, Lembeli alimpongeza Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Kikwete kwa maelezo kwamba maamuzi aliyochukua ni mazito, magumu na ya kijasiri ya kuanza kuwashugulikia wale wote wanaotuhumiwa kuhusika na vitendo vya ufisadi.
“Maamuzi yaliyofanywa na Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa CCM ni maamuzi magumu, yanayohitaji ujasiri wa hali ya juu wakati wa kikao cha Kamati Kuu ya CCM na baadaye Halmashauri Kuu ya CCM taifa mjini Dodoma hivi karibuni,”alisema.
Mbunge huyo alisisitiza kuwa maamuzi hayo yamesaidia kujenga imani ndani ya chama hicho kikongwe hasa ilipoundwa sekretarieti mpya. Aidha, Lembeli alishauri ili kupata dawa ya kudumu kwa mafisadi ni vyema taifa likarejesha Azimio la Arusha kwani hivi sasa viongozi hawazingatii maadili na miiko ya uongozi.
Alieleza kuwa kitendo cha mafisadi hao kuachana na misingi iliyowekwa na vyama vya Tanu na Asp iliyowabana viongozi kuzingatia miiko ya uongozi, ndiyo chanzo cha kukigeuza CCM dodoki.
Aliahidi kuendeleza mapambano dhidi ya ufisadi bila woga na kuwataka wote walionyooshewa kidole wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM wakae kimya na wajirekebishe.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment