
Na Luqman Maloto
Mada hii isionekane ina dhamira ya kutoa njia za watu kuachana. Ningependa lichukuliwe kuwa ni somo sahihi kwa sababu ni muhimu kupeana njia zinazofaa.
Ieleweke kuwa, wajibu wa safu hii ni kuchambua masuala ya kimapenzi na kupeana mbinu za kukabiliana na changamoto zilizopo. Tunajikita kwenye eneo hilo kama ambavyo Babu wa Loliondo anavyosimamia utabibu wa magonjwa sugu matano.
Mada hii isionekane ina dhamira ya kutoa njia za watu kuachana. Ningependa lichukuliwe kuwa ni somo sahihi kwa sababu ni muhimu kupeana njia zinazofaa.
Ieleweke kuwa, wajibu wa safu hii ni kuchambua masuala ya kimapenzi na kupeana mbinu za kukabiliana na changamoto zilizopo. Tunajikita kwenye eneo hilo kama ambavyo Babu wa Loliondo anavyosimamia utabibu wa magonjwa sugu matano.
Pokea maneno yangu na uyasome kwa mtindo wa katikati ya mstari, mwishoni utajua namaanisha nini. Siwezi kushadadia utengano kwa maana najua athari na machungu yake.
Upo uhusiano ambao umelengwa kudumu, hasa kwa wanandoa. Kuna wengine hawana sura ya kudumu, wapo kwa muda kwa kuzingatia mazingira pamoja na kile kilichomo ndani ya nafsi zao.
Unaweza kujiuliza; kwa nini ufike wakati utake kuvunja uhusiano wako na mwenzako? Iwe kirafiki au kimapenzi, ipo wazi kwamba kuna sababu mbalimbali zinazoweza kuwafanya wahusika kuamua.
Yawezekana uhusiano wako na mpenzi wako au rafiki yako wa jinsia tofauti unakutia hasara, unakuharibia biashara, unakupunguzia heshima katika jamii au pengine uaminifu wako kazini.
Mathalan, mpenzi wako anafahamika kuwa ni kahaba. Inawezekana uhusiano wako na mwenzako unaidhuru nafsi yako. Mfano, mwenzio ana nguvu sana juu yako kiasi kwamba huwezi kusema “hapana” kwa lolote analokwambia.
Pengine kutokana na hali hiyo umekuwa ukilazimika kufanya mambo ambayo huyapendi na ambayo hayaendani na maadili.
Lakini pia yawezekana umeanza kumchukia mwenzako. Mazingira yamebadilika, kwa hiyo wewe na yeye hampatani tena. Unajitazama na kugundua kwamba ulivyo huendani naye. Ni matokeo ya kuchokana!
Uhusiano wowote unapoyumba, uwe wa kirafiki au kimapenzi, huwaweka wahusika katika wakati mgumu kiasi kwamba ni lazima mmoja achukue hatua ili aweze kuishi kwa amani na furaha ya kweli.
Hata hivyo, ikae akilini kwamba inauma mno kuachana na mtu unayempenda!
Kumaliza uhusiano wa kimapenzi au kirafiki si hatari, lakini la msingi ni kuhakikisha kuwa unamwacha mwenzako akiwa hajaathirika kisaikolojia kwa namna yoyote.
Kwa sababu hiyo unapaswa kujifunza njia sahihi ya kumaliza uhusiano wako na mwenzako inapobidi.
Kuna jamii inaweza kuthubutu kusema, unapochoshwa na mtu, mchukue uende naye mahali kisha umueleze kwa uwazi kuwa hutaki tena kujihusisha naye kwa sababu moja, mbili, tatu.
Hata hivyo, hilo si jambo rahisi kwa wengi. Badala ya kukabaliana na mtu ana kwa ana na kumweleza kuwa humhitaji tena. Zipo njia za kirafiki ambazo unaweza kuzitumia bila kusababisha matatizo yoyote ya kisaikolojia.
ANDAA SABABU ZAKO
Unapotaka kumbwaga rafiki yako au mpenzi wako ambaye hujampa ahadi yoyote ya kuishi naye katika ndoa, anza mchakato kwa kuweka bayana sababu zinazokufanya utake kuachana naye.
Hakikisha kuwa, sababu unazoziweka ni zile ambazo mpenzi wako huyo hatapata namna ya kuzipinga.
Zitengeneze sababu hizo kwa kuzingatia mtazamo wako mwenyewe, na si wa kwake ili hatimaye kusiwe na mwanya kwamba atajirekebisha na mtaendelea kuwa pamoja.
Namna hii utakuwa unayaangalia zaidi maslahi yako mwenyewe na iwapo utalazimika kumweleza mwenzako ni kwa nini unataka kumaliza uhusiano wako na yeye, sababu zako hazitaonekana kama shambulio kwake yeye mwenyewe wala tabia yake.
USITHUBUTU KUWASILIANA NAYE
Utakapokuwa umeweka wazi sababu zako na kuziamini, weka mkakati kuwa hutaanzisha tena mawasiliano na mwenzako.
Jiwekee msimamo kuwa hutampigia simu, kumtumia ujumbe wa simu wala barua pepe na kadhalika, ila utajibu tu yeye atakapoanzisha.
Unapomwalika mtu, kumpigia simu au kumtumia ujumbe ni kama unamtia moyo na kumfanya aamini kuwa unampenda na kumjali.
Kama mhusika ni mtu mwenye fahamu atashtuka kuwa, jitihada zote anafanya yeye na wewe uko kimya. Akitafakari atagundua kuwa hauko naye tena.
AKIKUITA KATAA
Iwapo kweli umedhamiria kumaliza uhusiano wako na mwenzako, jaribu kukataa mialiko anayokupa, mathalan kwa ajili ya chakula cha pamoja cha mchana. Pia kama atasema atakufanyia jambo fulani, kataa kiaina.
Fanya vivyo hivyo kwa matukio yote ya kijamii. Kataa mialiko kwa njia ambayo hatakushtukia haraka kuwa humhitaji tena, bali aje kushtuka baadaye atakapojumlisha matukio.
Katika hatua za awali, hii itamaanisha kuwa utakosa kwenye matukio fulani ambayo wewe mwenyewe ungependelea kuyahudhuria. Huna la kufanya maana umeazimia kumaliza uhusiano na mpenzi au rafiki yako.
Unapotaka kupeleka ujumbe kwa mpenzi wako kuwa hayuko tena moyoni mwako, lazima tu ujitolee kupata hasara katika baadhi ya mambo. Kumbuka kuwa huhitaji tena uhusiano na mwenzako.
PUNGUZA MWITIKIO WAKE
Kuna wakati ambapo rafiki au mpenzi wako atafanya au kusema jambo na wewe utatakiwa kuonesha mwitikio. Kama umeshadhamiria kuachana naye, onesha mwitikio wa shingo upande.
Kama mhusika atabaini jinsi ulivyoitikia shingo upande, utakuwa umepeleka ujumbe maridhawa, kuwa huna tena furaha na uhusiano wenu na kwamba unahisi ni wakati muafaka wa kumaliza mambo.
Kuna mazingira ambayo hutaepuka kumwitikia mpenzi au rafiki unayetaka ‘kumpiga chini’. Kwa sababu hiyo, ndiyo maana unapaswa kumwitikia lakini katika hali ambayo inaonesha kwamba huna habari naye tena.
Itaendelea wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment