Watua kwa ndege ya kukodi
Kocha Patrick Phiri wa Simba amesema wapinzani wao katika mechi ya kesho ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika, TP Mazembe wanaihofia timu hiyo ya Msimbazi na kwamba kama wenyeji "watakomaa" watawavua ubingwa wa Afrika wageni hao.
Phiri alisema mechi ya kwanza baina yao iliyofanyika mjini Lubumbashi wiki mbili zilizopita imewaachia hofu TP Mazembe baada ya Simba kucharuka katika dakika za mwisho na kupata goli moja na kuonekana kama wangeweza kuongeza magoli zaidi licha ya kulala kwa 3-1.
Mzambia huyo alisema kwamba wageni hao hawawezi kuwa na amani hata kidogo katika mechi ya leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, na kwamba kauli za kuisifu Simba zilizotolewa na miamba hao wa Afrika baada ya mechi ya awali zinathibitisha kuwa "presha" iko juu.
Akiongea na waandishi wa habari jana, Phiri alisema kuwa atakifanyia mabadiliko kikosi chake cha kwanza kwa kuwa atawakosa baadhi ya wachezaji waliokuwepo kwenye kikosi kilichocheza Lubumbashi.
“Nimefanyia marekebisho makosa yaliyojitokeza kwenye mchezo wa kwanza na pia kikosi kitakachocheza kesho kitakuwa na mabadiliko kidogo ukilinginisha na kikosi kilichocheza Lubumbashi,” alisema Phiri.
Alisema kuwa mmoja wa wachezaji atakaowakosa kesho ni pamoja na Amri Kiemba ambaye ni majeruhi.
Phiri alisema kuwa ana matumaini ya kufanya vizuri kesho hasa kutokana na uwezo mkubwa waliouonyesha kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Lubumbashi licha ya kwamba Simba ilifungwa.
“Simba na TP Mazembe ni kama mwanafunzi na mwalimu kwa kuwa wenzetu wana uwezo na uzoefu mkubwa kwenye mashindano ya kimataifa... lakini watu wajue kuwa mwanafunzi anaweza kumfundisha mwalimu wake, tutawashangaza watu Jumapili,” alisema Phiri.
Mshambuliaji wa Simba, Mussa Hassan Mgosi alisema wachezaji wako tayari kufia uwanjani ili kuhakikisha wanaivua ubingwa timu hiyo walivyofanya kwa Zamalek ya Misri mwaka 2003.
Mabingwa watetezi wa Afrika mara mbili mfululizo, Mazembe walitua jana saa 12:00 kwa ndege ya kukodi wakiwa na watu 32 ambao walijumuisha wachezaji na maafisa wengine wa timu hiyo. Kisha wakakataa kufikia katika hoteli waliyopangiwa na wenyeji na kwenda kufikia Kempinski.
Simba pia mjini Lubumbashi walikataa hoteli waliyokuwa wamepangiwa na Mazembe.
Awali, Mazembe ambao walificha ujio wao hata katika ubalozi wao nchini, walidaiwa kwamba wangewasili saa 5:00 asubuhi na hivyo kusubiriwa na waandishi pamoja na Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, bila ya mafanikio.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment