Vijana wakazi wa eneo la Polisi Ufundi barabara ya Kilwa Dar es Salaam wakisaidia kuweka vyombo ndani ya nyumba ambayo ilikuwa inakaliwa na mtu asiyekuwa askari baada ya gazeti hili kuandika habari hizo Aprili 27. Nyumba hiyo sasa amepewa askari mhusika. (Picha na Yusuf Badi).
HATIMAYE askari Polisi aliyekuwa akilala nje na familia yake kwa mwezi mmoja baada ya kuzuiwa kuingia ndani ya nyumba aliyopewa, jijini Dar es Salaam amekabidhiwa nyumba hiyo chini ya usimamizi wa Mkuu wa Polisi wa Kituo cha Kati (OCS), Pili Mande.
HABARILEO limemshuhudia mke wa askari huyo, Sofia Gapile, akiingiza samani zake ndani ya nyumba hiyo, huku samani za aliyekuwa akizuia nyumba hiyo kwa nguvu, mtoto wa Sajini Pascal zikitolewa nje na kuhifadhiwa katika stoo ya nyumba za Polisi eneo hilo.
Kabla ya kukabidhiwa haki yake, polisi huyo na mkewe walikuwa wakilala kwenye mkeka nje ya nyumba hiyo, huku wanawe wawili wakiombewa kwa majirani na samani zake zikiharibiwa na mvua nje.
Sofia amesema, mumewe ambaye ni askari wa kituo cha Polisi Kati tangu Machi 16 aliomba kuishi katika nyumba za Polisi zilizoko Ufundi Temeke kwa kufuata taratibu zote na kukubaliwa na wahusika.
Nyumba hiyo namba 24 awali ilikuwa ikitumiwa na Sajini Pascal na familia yake kabla ya kujenga nyumba yake katika eneo la Tabata Kinyerezi, Dar es Salaam, na kuhamia huko.
Sofia amesema, baada ya askari huyo kuondoka, walihamishia samani zao kwenye nyumba hiyo na kukuta mtoto wa kiume wa Pascal na askari mwingine wa kituo cha Sitakishari wakiishi hapo.
Amesema, wenyeji hao walipotakiwa kuondoka, walikaidi na kuendelea kuishi ndani ya nyumba hiyo huku familia hiyo ikilala nje kwa kukosa mahali pa kuishi.
Kutokana na mazingira hayo magumu ya familia hiyo, mume wa Sofia alilazimika kubadilishia nguo chooni ili awahi kazini.
Lakini, baada ya HABARILEO kuandika habari hizo wiki hii, OCS Mande alifika katika eneo hilo leo saa 4.30 asubuhi akifuatana na Mkuu wa kambi na kuhakikisha kufuli lililokuwa likining’inia kwenye mlango wa nyumba hiyo linavunjwa na familia ya askari huyo inaingiza vitu ndani.
Wakati ujumbe huo wa Polisi ulipofika eneo hilo, haukumkuta mtoto huyo na alipopigiwa simu ili afike kuchukua mali yake, aliwaelekeza samani hizo zitolewe na kuwekwa stoo.
CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment