Advertisements

Tuesday, May 31, 2011

Dk. Slaa, Lema wanusurika kusota rumande

UPEPO wa kuswekwa rumande jana nusura uwakumbe Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa na Aquelini Chuwa mkoani Arusha baada ya polisi kutaka kuwakamata walipokwenda kujisalimisha mahakamani. 

Wiki iliyopita Mei 27, Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Arusha Charles Magesa alitoa 
amri ya kukamatwa kwa Lema, Dk. Slaa, Freeman Mbowe, Philemon Ndesamburo na Josephin Slaa kwa kushindwa kuhudhuria mahakamani bila ya taarifa yoyote na kuamuru polisi kuwakamata popote walipo.
 

Sakata hilo lilianza saa 8.15 mchana wakati watuhumiwa hao waliporudi mahakamani saa 
saba baada ya kufika saa 3 asubuhi na kuambiwa kurudi muda huo. 

Baada ya kukaa kwa muda wa saa 1.15 mawakili wa washitakiwa hao Method Kimomogolo na Albart Msando walimwona Hakimu Mfawidhi kumjulisha kuwa watuhumiwa Lema na Slaa walikuwa nje na walikwenda kujisalimisha, hatua iliyopingwa na Hakimu Magesa. 

Kwa mujibu wa Msando, Hakimu Magesa alisema yeye alishatoa amri ya watuhumiwa wote 
kukamatwa kwa kudharau mahakama wao na wadhamini wao hivyo kilichotakiwa ni kukamatwa na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi na baadayekuletwa mahakamani. 

Wakili Msando alisema, sababu hiyo iliungwa mkono na Wakili wa Serikali Mwandamizi EdwinKakoraki na kupiga simu polisi kuwaita ili wawakamate Lema, Slaa na Chuwa ili waende 
kwanza rumande na baadaye kuletwa mahakamani kujibu shitaka la kuidharau mahakama. 

Muda mfupi tu magari mawili ya polisi yaliwasili yenye namba za usajili PT 1177 na PT 1414 
yakiwa na askari wasiopungua 12 huku wakiwa na silaha tayari kuwapeleka watuhumiwa hao rumande. 

Ubishi ulizuka kwa Dk. Slaa na Lema kugoma kwenda polisi na kudai kuwa wao wamekwenda 
wenyewe mahakamani kujisalimisha baada ya kutolewa hati ya wao kukamatwa “hivyo 
mwenye mamlaka ya sisi kukamatwa kwenda rumande ni hakimu mwenyewe na sio nyie polisi hapa hatuondoki,” alisema Dk. Slaa. 

Wakati malumbano hayo yakiendelea mawakili wa washitakiwa walikuwa katika chumba cha 
hakimu Magesa wakimsihi asikilize sababu za watuhumiwa kujisalimisha; alikubali kusikiliza 
hoja zao. 

Alisikiliza hoja za upande wa utetezi kuhusu kutokufika mahakamani kwa wateja wao na kutolewa sababu mbalimbali, lakini upande wa serikali uliomba muda kupitia uhalali wa vyeti kwa watuhumiwa ambao walidai kwamba walikuwa wagonjwa. 

Hakimu huyo aliahirisha kesi hiyo hadi leo saa 7 mchana ili asikilize sababu za wakili wa serikali na kutoa uamuzi wa jumla ya juu ya kufuta dhamana na kutofuta dhamana kwa washitakiwa kwa kukiuka kuhudhuria mahakamani bila ya sababu za msingi.


CHANZO:HABARI LEO

No comments: