Advertisements

Tuesday, May 31, 2011

Rage: Tumekubali kipigo Misri

Mwenyekiti wa klabu ya Msimbazi, Ismail Aden Rage
Uongozi wa klabu ya Simba umesema kuwa umekubaliana na kipigo cha 3-0 walichopata kutoka kwa Wydad Casablanca ya Morocco katika mashindano ya klabu bingwa barani Afrika, na hauna mpango wa kukuta rufaa yoyote kwa Shirikisho la soka Afrika (CAF) dhidi ya mchezo huo.
Awali kulikuwa na taarifa kuwa Simba wamekata rufaa CAF kupinga kucheza na Wydad mechi maalum ya kuwania nafasi ya kucheza hatua ya makundi baada ya CAF kuitupa nje ya mashindano timu ya TP Mazembe.

Akizungumza na NIPASHE jana, Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, alisema kuwa kwa sasa wanaanza maandalizi kwa ajili ya ushiriki wa timu hiyo katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kutolewa na Wydad.
"Hakuna kitu kama hicho, Simba hatutakata rufaa yoyote, tumepoteza mchezo wetu dhidi ya Wydad sasa hivi tunaanza maandalizi kwa ajili ya Kombe la Shirikisho, suala la rufaa ni maneno tu ya watu," alisema Mtawala.
Aidha, alisema kuwa kikosi cha timu hiyo kimerejea nchini jana alfajiri na leo jioni wataanza mazoezi kujiandaa kwa ajili ya mashindano hayo ya pili kwa ukubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika.
Alisema kuwa kutolewa kwao na Waydad kumechangiwa na kukosa muda wa kutosha wa maandalizi baada ya wachezaji kukusanywa wakitokea kwenye mapumziko ya mwisho wa hivyo, wameona ni muhimu kutovunja kambi ili wapate muda mrefu wa kujiandaa na mechi yao ya Kombe la Shirikisho dhidi ya DC Motema Pemba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Juni 12, ambapo mechi ya kwanza baina yao itachezwa ugenini.
Mwenyekiti wa klabu hiyo ya Msimbazi, Ismail Aden Rage, alisema kuwa wamekubaliana na kipigo hicho kutoka kwa Wydad lakini anaamini kocha wa timu hiyo, Mosses Basena, atayafanyia kazi mapungufu yaliyoonekana kwenye mchezo huo uliochezwa katika uwanja wa ugenini kwa kila upande nchini Misri.
Katika mchezo huo maalum dhidi ya Wyadad uliofanyika Jumamosi kwenye uwanja wa PetroSport jijini Cairo, Misri, Simba ilirejea katika mashindano hayo makubwa zaidi kwa ngazi ya klabu Afrika kwa ushindi wa mezani baada ya CAF kuona kuwa ni kweli TP Mazembe ilimchezesha isivyohalali mchezaji Javier Bakungu, ambaye alikuwa bado ni mchezaji halali wa Esperance ya Tunisia, katika kipindi ambacho timu hiyo ya Congo ilikuwa tayari imeshatinga hatua ya makundi kwa kuitoa Wydad.
CHANZO: NIPASHE

No comments: