Advertisements

Tuesday, May 31, 2011

Padri adaiwa kubaka mwanafunzi, asakwa

Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linamtafuta Padri wa Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro, Parokia moja ya jimbo hilo kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi mwenye umro wa miaka 20 anayesoma kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Alfa, Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Adolphina Chialo, alimtaja Padri huyo, lakini kwa sababu za kimaadili na baada ya kushindwa kumpata kwa simu yake ya mkononi, tunalisitiri jina lake kwa sasa.

Alidai taarifa za tukio hilo ziliripotiwa na mwanafunzi huyo ambaye kwa sasa jina lake linahifadhiwa, Mei 28, mwaka huu akidai kufanyiwa kitendo hicho jijini Dar es Salaam Machi 30, mwaka huu. Hata hivyo, tukio hilo halikuripotiwa kwenye kituo chochote cha polisi mkoani Dar es Salaam.
Chialo alisema kwa mujibu wa simulizi za mwanafunzi huyo, Padri huyo alimwita (mwanafunzi) jijini Dar es Salaam ili ampatie fedha za masomo ya ziada.
Akizungumza na NIPASHE mwishoni mwa wiki iliyopita mwanafunzi huyo ambaye ni yatima alidai Padri huyo alianza kufadhili masomo yake alipoanza kidato cha tano baada ya yeye kuomba msaada kupitia gazeti moja la kila siku.
Mwanafunzi huyo alidai Padri huyo alikuwa akimsaidia bila kuonyesha dalili zozote za kumtaka kimapenzi, hivyo alipomwita aje jijini Dar es Salaam hakuwa na shaka kuwa angeweza kumfanyia kitendo hicho.
Alidai Padri huyo alimpigia simu na kumtaka kwenda kuchukua fedha za masomo ya ziada eneo la Tiptop Mazense, Dar es Salaam.
“Niliwasiliana naye kwa simu nikiwa Dar akaniuliza mbona hujachukua fedha za tuisheni (tuition) njoo hapa Manzese Tiptop uchukue, nilipofika akaniambia twende huku juu nikamwambia wapi akasema siwezi kukupa fedha hadharani, mimi si kama baba yako,?” alidai mwanafunzi huyo.
Mwanafunzi huyo alidai kuwa alipofika chumbani kwa Padri huyo alifunga mlango kisha kumfanyia kitendo hicho na alimsihi asiseme kwa mtu yeyote kwa kuwa atamdhalilisha yeye pamoja na Kanisa kwa ujumla.
Mwanafunzi huyo aliliambia gazeti hili kuwa anahofia afya yake na aliomba msaada kwa mashirika ya kutetea haki za binadamu.
Alipoulizwa ni kwa nini kwanza imemchukua muda mrefu, takribani mwezi mzima kutoa taarifa hizo polisi, na kwa nini hakutoa taarifa hizo polisi jijini Dar es Salaam baada ya kufanyiwa unyama huo, alisema aliombwa na kubembelezwa sana na Padri huyo asilifichue tukio hilo kwa yeyote.
Hata hivyo, alisema baada ya kukaa kwa muda wa mwezi mmoja sasa ameanza kuwa na wasiwasi juu ya afya yake ndiyo maana ameripoti polisi.
Kuna habari kwamba kumekuwa na juhudi za kuzima tukio hilo lisiripotiwe kokote zinazodaiwa kushirikisha watu wa kanisa na baadhi ya askari polisi.
CHANZO: NIPASHE

No comments: