Tuesday, May 3, 2011

Mchungaji Mwasapila ahofia maisha yake

Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwasapila
Mussa Juma, Samunge
MCHUNGAJI mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwasapila, amesema huduma anayofanya ya kutoa tiba ya magonjwa sugu, imeweka maisha yake hatarini.Akizungumza na mamia ya watu jana kabla ya kuanza kutoa kikombe cha dawa, Mchungaji Mwasapila alisema wanaotishia maisha yake ni makundi ya watu waliokuwa wanatoa tiba za uongo kutibu maradhi mbalimbali.

"Wanachukia kusikia natoa tiba ya magonjwa hapa, sasa wanajipanga kila siku kuniangamiza ,lakini Mungu ananilinda kila kona sambamba na vyombo vya dola vilivyopo hapa na hawataniweza hadi Mungu anichukue mwenyewe," alisema Mwasapila.

Alisema baadhi ya watu hao wanaotishia maisha yake, wamekuwa wakitoa tiba za uongo na wengine ni wagonjwa, hivyo wanajua baada ya muda mfupi hawatakuwapo duniani.
Mchungaji Mwasapila alifafanua kuwa, hata akifariki, Mungu hawezi kutoa uwezo wake kwa watu hao, kwani anapenda watu wanyeyekevu.

"Ndugu zangu kutokana na hali hii ndio sababu mmesikia matangazo kuwa ni marufuku kunishika mkono ili mnisalimie, naomba muelewe hivyo," alisema Mwasapila.
Alisema miongoni mwa makundi yanayompinga, ni wachungaji wanaowakataza waumini wao kwenda kupata tiba Samunge wakihofia kukosa sadaka.

"Naomba mje mpate kikombe cha tiba na mkipona mkawape sadaka yao, najua hilo ndio tatizo lao," alisema Mwasapila.Awali, Msaidizi wa mchungaji huyo ambaye ni Ofisa wa Serikali, Frederick Nisajile, alitangaza kuwa sasa ni marufuku kumsalimia mchungaji bila idhini kutokana na sababu za usalama.

Apiga marufuku fulana kuandikwa jina lake
Katika hatua nyingine, Mchungaji Mwasapila jana alitangaza kupiga marufuku kampuni za ndani na nje ya nchi kuendelea kutengeneza fulana zenye picha yake na kuuza bila idhini yake.

Akizungumza na Mwananchi jana, Mchungaji Mwasapila huku akitazama baadhi ya fulana zenye jina lake na sura yake zilipelekwa kuuzwa Samunge, alisema anawaomba watu hao kuacha kutumia jina lake kujinufaisha.

"Naomba unisaidie kueleza kuwa kama kuna kampuni au watu wanataka kutumia jina langu na picha kwenye biashara zao wawasiliane na mimi kwanza, la sivyo vyombo vya dola vitawashughulikia," alisema Mwasapila.

Kuhusu fulana ambazo jana zilikuwa zinauzwa Samunge, alisema kwanza wametengeneza bila ridhaa yake, lakini picha wanazotumia kutengeneza fulana hizo hazina ubora.
 "Waje hapa tuzungumze kuna ambao wamefika hapa na nimewapa utaratibu wa kufanya biashara yao nadhani tumeelewana,"alisema Mwasapila.

Fulana ambazo jana zilikuwa zikiuzwa Samunge, zilikuwa na picha ya mchungaji huyo na maneno mbalimbali ikiwamo 'Mchungaji wa ukweli wa Loliondo', 'Mtumishi wa Mungu Loliondo', 'Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokowae'.
 
Foleni yaanza 
kuongezeka Samunge
Foleni ya magari yanayokwenda Samunge kutoka ndani na nje ya nchi jana iliongezeka tena baada ya magari 500 kufika kijijini hapo.Kuongezeka kwa foleni hiyo kunatokana na kufunguliwa kwa vituo vya Bunda, Namanga, Mto wa Mbu, Babati na Arusha mjini ambavyo awali vilifungwa kutokana na tangazo la serikali kuwa huduma ya tiba ingeanza Mei 2, mwaka huu.
 
Kenya yaizidi 
Kete Tanzania
Katika hatua nyingine, wageni kutoka nje ya nchi wameanza kuingia nchini kupitia Nairobi, Kenya katika kile ambacho kinaelezwa ni kusambazwa matangazo kwenye mitandao kuwa, kama watu wanataka kwenda Samunge wapitie Uwanja wa Ndege wa Nairobi.

Raia wanne wa Rwanda, ambao juzi walifika Samunge walilalamikia upotoshaji huo, ambao uliwafanya kutumia zaidi ya siku nne kwa usafiri wa ndege kufika Samunge wakitokea Nairobi.
"Tumepata tatizo kubwa na usafiri kuunganisha ndege hadi kufika hapa, kumbe tungeweza kutoka Rwanda hadi Arusha na baadaye kufika hapa," alisema Fransis Ndeisabo.
 
Maabara haijaletwa Samunge
Uamuzi wa kupelekwa Samunge maabara inayotembea ambayo imekuwa ikitumiwa na Taasisi ya Taifa ya Uchunguzi wa Magonjwa (NIMRI), unategemea upatikanaji wa fedha na kukamilika kwa taarifa kikosi kazi kilichoundwa kufuatilia tiba kijijini hapo.Hamis Malebo wa NIMRI, ambaye alikuwa katika timu ya wataalamu wa sekta ya afya waliofika Samunge mwishoni mwa wiki alilieleza kuwa, mradi huo ni mkubwa kwani kunahitajika vitu vingi ikiwamo mafuta ya uhakika ya kuendesha mashine za maabara hiyo.
                                            
Serikali yapongezwa
kulipa uzito suala la Samunge
Watu kadhaa wanaoendelea kufika Samunge kupata tiba, wamepongeza hatua ya serikali kuipa uzito tiba hiyo kwa kuomba usaidizi wa utaalamu kutoka Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO)."Katika hili tunaipongeza serikali na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kweli wanalipa uzito suala la tiba ya Loliondo, kwanza kupima na kueleza haina madhara na sasa kuanza mchakato wa kutazama ubora wake," alisema Yohana Mahilu toka mkoani Mwanza.


CHANZO:MWANANCHI

No comments: