Na Elizabeth Mayemba
MABINGWA wa Ligi ya Ndani ya Uingereza 'Carring Cup', Birmingham City, wanatarajiwa kutua nchini Julai 5, mwaka huu, kucheza na Simba na Yanga, mechi maalumu za
kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru.
Birmingham, katika fainali za Carring Cup, iliifunga Asernal mabao 2-1 na kutwaa ubingwa huo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Rage, alisema timu yao itaanza kucheza na Birmingham Julai 7, mwaka huu, wakifuatiwa na Yanga Julai 12, ambapo mechi zote zitachezwa usiku.
"Birmingham watakuja na kikosi kamili, pia watakuwa wamefanya usajili wa wachezaji wao kwa ajili ya msimu ujao, na timu zetu zitatumia nafasi hiyo kuwapima wachezaji wao wapya waliowasajili kwa ajili ya msimu ujao wa ligi na michuano ya kimataifa," alisema Rage.
Alisema Mei 9, mwaka huu, Kocha Msaidizi wa Birminghamam, Endy Watson na daktari wa timu, Ian Mc Guiness, watafika nchini kukagua hoteli ya Kempiski ya Dar es Salaam na Uwanja wa Taifa, kwa ajili ya ujio wa timu hiyo.
Alisema timu hiyo itatua nchini na mashabiki 1,000, ambao kila mmoja atajihudumia kwa gharama zote kuanzia malazi, chakula hadi usafiri.
Mwenyekiti huyo alisema, pia wamefanya mazungumzo na Wizara ya Maliasili na Utalii ili wajue jinsi ya kuwapokea wageni hao, ambao watataka kuangalia vivutio vya utalii vya maeneo mbalimbali nchini.
Rage alisema, Simba mwakani ina mpango wa kuileta timu ya Liverpool, kama mambo yatakwenda vizuri.
CHANZO:MAJIRA
No comments:
Post a Comment