Tuesday, May 3, 2011

Wamiliki wa mabasi waomba radhi abiria

Wamiliki wa mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani wamewaomba radhi abiria kutokana na usumbufu walioupata Jumapili iliyopita, uliosababishwa na mgomo wa baadhi ya madereva.
Kutokana na mgomo huo, wamiliki hao wamesema watawachukulia hatua za kisheria madereva waliohusika kushawishi mgomo huo, huku wakidai kuwa wengine hawana mabasi wanayoendesha.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Dar es Salaam (DABOA), Severine Ngallo, alisema mgomo uliotokea Jumapili ulisababisha adha kubwa kwa wasafiri, ndugu na jamaa zao, hivyo wanaomba radhi na kuahidi kuwa hali hiyo haitatokea tena.

“Tungejua kuwa madereva wetu wamepanga kugoma, tusingukubali kukatisha tiketi na kusababisha usumbufu kwa abiria, kama walipanga kugoma wasingechukua mabasi nyumbani au gereji na kuyapeleka stendi, kilichofanyika ni uhuni” alisema Ngallo.
Aliongeza kuwa: “Kuna genge la baadhi ya madereva ndilo lililoshurutisha kufanyika kwa mgomo huo na ndiyo maana waliwapiga baadhi ya madereva waliokataa kushiriki mgomo, haukuwa mgomo wa madereva wote ndiyo maana baadhi ya mabasi tayari yalikuwa yameingia kwenye foleni ya kutoka”.
Wamiliki hao kutoka mikoa mbalimbali nchini waliokutana jana mjini Dar es Saaam, waliazimia kuchukua hatua za kisheria kwa wahusika wa mgomo huo na kuwa suala la mkataba kati ya mmiliki na dereva ni mambo binafsi, kwani hata mishahara inatofautiana kutokana na makubaliano yaliyofikiwa.
Katika hatua nyingine, mkutano wa wamiliki hao ulikuwa ukiendelea jana jioni ambapo wamiliki hao walikuwa wakijadili kuhusu mgomo kupinga kufungwa kwa mfumo wa udhibiti mwendo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: