ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 27, 2011

Mwanamke anayefaa kuolewa ni yupi hasa? - 2

HELLO! Ladies & Gents, sina shaka mtakuwa wazima na mpo tayari kupokea kile nilichowandalia. Karibuni sana darasani. Rafiki zangu, wiki iliyopita nilianza mada hii, ambayo msingi wake ni kuchambua aina mbili za wanawake; wa mjini na kijijini.

Kwa kuanzia, nilianza kueleza sifa mbili za mwanamke wa kijijini, yaani mabaya na mazuri au kwa maneno mengine, faida na hasara za mwanamke wa kijijini. Kutokana na ufinyu wa nafasi kama uonavyo msomaji wangu mpenzi, acha niende moja kwa moja kwenye muendelezo wa mada hii.


UKWELI KUHUSU WANAWAKE WA MJINI
Inaelezwa kwamba, wanawake wengi wa mjini ni wajanja wa kila kitu, uelewa, akili na hata utafutaji. Wengi wameelimika (angalau wamefika kidato cha nne na kuendelea). Ambao wamesoma vyuo mbalimbali wana nafasi kubwa ya kuajiriwa katika kampuni mbalimbali jambo linaloweza kuweka mgawanyo wa kutimiza majukumu ndani ya nyumba.

Mwanamke huyu ana msimamo, siyo rahisi kuyumbishwa, anatumia akili zaidi kuliko nguvu. Hana papara na mambo yake, hupangilia pointi zake katika kumkosoa mwanaume. Mchakarikaji, mchangamfu, anajua mahaba, akili yake imepanuliwa na utandawazi wa ukuaji wa Sayansi na Teknolojia.

Siyo ‘mshamba’, anajua kila kitu, siyo mgeni sana na wanaume (hasa walaghai), ni muwazi, mwepesi kushauri/kushauriwa na liwazo la kweli unapokuwa mgonjwa. Mwanamke huyu haogopi kukushauri unapokwama (hata kama hujamwomba afanye hivyo).

Pia baadhi yao wanapenda kujiendeleza kielimu jambo ambalo linazidi kuwapa nafasi ya kuwa wake bora zaidi. Hoja hujibiwa kwa hoja. Hutumia vitu vya kisasa kuhakikisha penzi linazidi kuwa imara. Anatambua haki zake kama mwanamke, lakini pia anajua wajibu wake kwa mumewe.

Kumbuka kuwa, siyo kila nilichoandika hapo juu kipo kwa kila mwanamke wa mjini, wengine huwa navyo vyote, zaidi au pungufu lakini kwa wastani wanawake walio wengi huwa na sifa hizi.

Hata hivyo, ukiachana na sifa hizo, yapo mabaya ya wanawake wa mjini. Baadhi yake ni wale wanaotumia vibaya utandawazi hujikuta wameharibika na hivyo kuwa na tabia chafu. Mitandao ya simu za mikononi na intaneti zinatajwa kama vyombo vinavyotumiwa na baadhi ya wanawake hao kufanya ufuska.

Ni wanawake wa gharama, wanapenda kutolewa out, disko na kumbi mbalimbali za burudani kila mwisho wa wiki. Kama akizoeshwa ndiyo huwa hatari zaidi, kwani siku asipotolewa, huwa ugomvi mkubwa, maana ameshachukulia kama sehemu ya maisha yake ya kimapenzi.

Wakati mwingine ni wabishi, wanaweka fedha mbele, wakiamini fedha ni kila kitu katika mapenzi. Baadhi yao huwa na wanaume kwa ajili ya kujipatia fedha tu, na siyo ajabu siku zikiisha ikawa ndiyo mwisho wa mapenzi.

Mara nyingi wanawake hawa wamezoea maisha mepesi, siyo rahisi sana kukabiliana na mikikimikiki ya maisha. Kwa maneno mengine, huwa hawawezi kuishi katika mazingira ya shida au mabadiliko ya mazingira/tabia nchi.

Tatizo lingine kwa wanawake hawa ni mavazi yao, mara nyingi mavazi yao hayana staha na hata kama ukimweleza juu ya hilo, huwa mgumu sana kubadilika.

Siyo werevu wa kukabiliana na vishawishi (hasa waliopo maofisini). Ni wepesi kushawishiwa kwa ahadi ndogo ndogo au mvuto wa kimahaba wa wanaume watanashati.

Ni wajanja wa kutengeneza mambo, wanaweza kuwa wamefanya kitu, lakini wakakudanganya kwamba hawajafanya, hata kama ni kwa kutoa machozi! Huyu ni mkali wa kufanya usanii na usishtukie kirahisi.

Umeona rafiki? Lakini usisahau kwamba, siyo kila mwanamke anaweza kuwa na tabia nilizoanisha hapo juu. Wengine wana baadhi, zaidi au pungufu lakini kwa wastani wengi wana tabia hizo.

Sina shaka sasa, umeanza kuelewa japo kidogo kuhusu wanawake hawa wanaoishi katika mazingira tofauti. Swali la msingi sasa ni je, nani kati ya hawa anaweza kuwa mke bora zaidi ya mwenzake?

Je, kuna ukweli kwamba wanawake wa kijijini wakiolewa na wanaume wa mjini hubadilika? Je, mwanaume wa kijijini anaweza kuoa mjini na kumchukua mwanamke huyo kwenda kuishi naye kijijini? Usikose sehemu ya mwisho ya mada hii wiki ijayo, ambayo itakuwa na majibu ya maswali yote hayo.

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi ambaye anaandikia magazeti ya Global Publishers, ameandikia vitabu vya True Love na Let’s Talk About Love vilivyopo mitaani.
NB: Kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wetu, leo tena tumeshindwa kuendelea na LOVE MESSAGES na FROM ME TO U, hadi mambo yatakapokuwa sawa.

No comments: