ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 27, 2011

Simba watua Misri, wajifua kwa siri

Wachezaji wa Simba leo wanatarajia kufanya mazoezi ya siri katika uwanja wa hoteli ya kimataifa ya Paradise waliyofikia ili kuwaficha wapinzani wao mbinu watakazozitumia katika mechi yao itakayofanyika kesho ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco.
Mechi hiyo kati ya Simba ya Dar es Salaam na Wydad Casablanca itakuwa ni moja na mshindi atafuzu kuingia katika hatua ya makundi ya mashindano hayo yanayosimamiwa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).

Akizungumza kwa njia ya simu na NIPASHE jana jioni, Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, alisema kuwa kikosi cha timu hiyo kiliwasili jijini Cairo jana saa 12:45 asubuhi (sawa na saa 1:45 za hapa Tanzania) kikiwa salama na kilipokelewa vizuri na wenyeji wao maafisa wa ubalozi wa Tanzania nchini Misri.
Mtawala alisema kuwa wachezaji jana jioni walifanya mazoezi mara moja tu kwenye uwanja wa Petrosport ambao ndio utatumika katika mchezo wa kesho lakini leo hawataenda kufanya mazoezi kwenye uwanja huo.
Alisema kuwa kocha wa timu hiyo, Mganda, Moses Basena, ameamua kutoipeleka timu yake kesho na badala yake watabaki katika hoteli waliyofikia kumalizika mbinu za kiufundi.
"Mwalimu (Basena) ameamua leo wachezaji wakauone na kuuzoea uwanja utakaotumika, lakini kesho (leo) hawataenda, tutatumia uwanja wa hapa hapa hotelini ambao ni mkubwa na una hadhi pia, kuna vitu kocha anataka kuwaeleza wachezaji bila ya watu wengine kuona," alisema katibu huyo.
Aliongeza kuwa kila kitu walichopanga kinakwenda vizuri na wachezaji wana morali ya juu na wanatarajia kuweka rekodi kwenye mashindano haya baada ya kushinda rufaa yao.
Alisema pia baadhi ya Watanzania waliopo jijini Cairo walijitokeza kuipokea timu na wanatoa ushirikiano kwa sababu wanataka kuona inashinda na kuwaondoa Waarabu hao kwenye mashindano hayo.
Alisema kwamba wachezaji wote 17 walioondoka wako vizuri na hakuna majeruhi na kilichobaki ni kukamilisha jukumu walilonalo la kupambana ili kusonga mbele.
Mechi hiyo kati ya Simba na Wydad Casablanca itaanza saa 1:00 usiku kwa saa za Tanzania na timu itakayofungwa itahamia kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho.
Wakati huo huo, kocha wa Simba, Mosses Basena, amesema kuwa licha ya kikosi chake kuwakosa nyota wake wawili wa kikosi cha kwanza, Mbwana Samata na Patrick Ochan, waliosajiliwa na TP Mazembe, wachezaji waliopo wana uwezo wa kupata matokeo ya ushindi wanayoyahitaji dhidi ya Wyadad Casablanca.
Akizungumza na NIPASHE muda mfupi kabla ya timu hiyo haijaondoka kuelekea Cairo kwa ajili ya mchezo huo unaofanyika kwenye uwanja huru, Basena, alisema kuwa anafahamu kama Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lingeruhusu Simba iwatumie wachezaji hao, Wekundu hao wangekuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kufanya vizuri.
"Kama wangeruhusiwa kikosi kingekuwa na nguvu zaidi, lakini tulijipanga kwa maamuzi haya, wachezaji waliopo bado wananafasi ya kufanya vizuri kama watafuata maelekezo yangu," alisema Basena.
CHANZO: NIPASHE

No comments: