.jpg)
Meneja Mawasiliano ya shirika la TANESCO, Badra Masoud
Shirika la Umeme nchini (Tanesco), limetangaza kufuta mgawo wa umeme na kuanzia leo nishati hiyo itaanza kupatikana kama kawaida kwenye maeneo yote nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Meneja Mawasiliano ya shirika hilo, Badra Masoud, hali hiyo imetokana na kukamilika kwa matengenezo ya visima vya kuzalisha gesi asili katika kisiwa cha Songosongo.
Alisema visima hivyo vilanza kufanyiwa matengenezo Mei 19 hadi jana hali iliyosababisha upungufu mkubwa wa umeme katika gridi ya taifa na kuwaathiri watumiaji wa nishati hiyo.
“Upungufu huo ulitokana na visima na mitambo ya gesi asili iliyopo katika kisiwa cha Songosongo mkoani Lindi kuzimwa na wamiliki wake Pan African Energy Tanzania Ltd kwa ajili ya ukaguzi na ukarabati,” Masoud alisema katika taarifa yake hiyo.
Alisema lengo lilikuwa ni kuboresha viwango vya gesi inayozalishwa na kusafirishwa kutoka kisiwa hicho hadi Dar es Salaam kwa ajili ya kufua umeme na kutumiwa viwandani.
Alitaja vituo ambavyo hutumia gesi asili ya Songosongo kuzalisha umeme kuwa ni Songas, Ubungo Gas Plant na Tegeta Gas Plant.
Alisema umeme wa gesi huchagia karibu nusu ya umeme unaofuliwa kwenye vituo vyote nchini.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kina cha maji katika bwawa kuu la Mtera ni mita 691.08 juu ya usawa wa bahari na kina cha juu kwenye bwawa hilo ni mita 698.50 na kina cha chini ni mita 690.00 juu ya usawa wa bahari.
Hata hivyo, shirika hilo limesema bado kuna upungufu wa megawati 182.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment