ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, August 30, 2011

CCM, Chadema anga kwa anga Igunga


*CC YA  CCM WAMPITISHA  ALIYEKUWA MPINZANI WA ROSTAM, MKAPA KUZINDUA KAMPENI
Leone Bahati
KAMATI Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imemtangaza Dk Dalaly Kafumu kuwa mgombea wake katika uchaguzi mdogo wa Igunga huku pia kikitangaza kutumia helikopta kupiga kampeni za anga kwa anga ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha jimbo hilo haliangukii kwenye himaya ya upinzani.

Hatua ya CCM kutangaza kutumia helikopta inakuja wakati tayari Chadema, nacho tayari kikiwa kimetangaza kutumia usafiri huo wa anga kufika maeneo mengi katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2 kuziba nafasi ya Rostam Aziz, aliyejiuzulu wadhifa huo mnamo mwezi Julai.

Wakati vyama vingine vya upinzani vikiwa vimemaliza mchakato wa kupata wagombea wao, jana CC ya CCM ilikutana jijini Dar es Salaam chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete, ambayo pamoja na mambo mengine ilimtangaza Dk Kafumu ikiwa ni kukamilisha mchakato huo ulioanzia ngazi ya wilaya.

Utaratibu wa CCM, mgombea ubunge huanza kupigiwa kura na wajumbe wa kuanzia wilaya kisha mkoa na  kutoa alama pasipo kukata jina hata moja na mwisho CC chini ya mwenyekiti, hufanya maamuzi ya mwisho.

Hadi sasa tayari CUF wamempitisha Leonard Mahona, ambaye alichuana na Rostam mwaka jana na kupata kura 11,000, Chadema ni Joseph Kashindye, Moses Edward (TLP) na John Maguma wa Sau, huku uchukuaji fomu ukiwa tayari umeanza tangu Agosti 24 na kutarajiwa kukamilika Septemba sita.

Vyama vya upinzani vikikamilisha mchakato na uchukuaji fomu ukiwa umeanza, jana Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa wa CCM, Nape Nnauye, ilitangaza uamuzi huo wa CC wa kumpitiisha Dk Kafumu, ambaye tayari aliwahi kugombea na Rostam mara mbili katika kura za maoni ndani ya chama bila mafanikio. 

Nape alitamba  kwamba CCM inaingia  kwenye uchaguzi huo ikiwa na matumaini makubwa ya kushinda huku  kauli mbiu ikiwa ni, "Tumethubutu, tumeweza na tunasonga mbele.”

Mkapa kuzindua kampe

Alifafanua kwamba mbali ya uamuzi wa kumpitisha Dk Kafumu, kikao hicho cha CC kilimpitisha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa kuzindua kampeni za chama hicho, zitakazoanza mwezi ujao.

“Kampeni hizo zitazinduliwa na Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Benjamini Mkapa wakati muafaka wa kampeni utakapowadia,” alisema Nape na kuongeza tambo akisema CCM itashinda uchaguzi huo kwa kishindo.


Sababu za kushinda wanazo

Alitaja sababu nne ambazo alizielezea ni miongoni mwa nyingi zinazokipa chama hicho tawala jeuri ya  ushindi kwenye uchaguzi huo, ambazo ni pamoja na tathmini waliyoifanya katika siku za karibuni na kubaini wanachama wake katika jimbo hilo wana mshikamano mkubwa na mapenzi kwa chama chao.

Nape aliitaja  sababu nyingine ni kwamba, katika uchaguzi wa kura za maoni walizofanya siku za karibuni jimboni humo zilionekana kuwa na utulivu na hakukuwepo na makundi yenye msuguano kama ilivyokwishawahi kutokea kwenye baadhi ya majimbo ambayo CCM iliyapoteza kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Katika kudhihirisha hilo, Nape alisema hata wagombea walioshindwa kwenye kura za maoni walikuwa jijini Dar es Salaam na waliahidi kuwa watashirikiana na Dk Kafumu katika kufanikisha ushindi wa CCM.

“Katika kufanikisha kampeni za CCM, wanachama waliowania kuteuliwa katika nafasi hiyo wameahidi watashiriki kikamilifu katika kampeni hizo,” akisema hiyo ni ishara ya mshikamano wa wana CCM Igunga.

Wagombea wanaotarajia kumuunga mkono DK Kafumu ambaye aliibuka mshindi wa kura za maoni, 588, ni aliyemfuatia kwa karibu Jafari Omari aliyepata 193 na Shams Brahamu,  aliyepata kura 38 kati ya wagombea jumla 13 walioshiriki uchaguzi huo kuomba ridhaa ya chama hicho tawala na kikongwe barani Afrika. 

Nape akisisitiza sababu za ushindi katika uchauguzi huo, alisema ni pamoja na  CCM kuwa na mizizi imara iliyojikita katika vitongoji vyote vya jimbo hilo, tofauti na vyama vya upinzani.

“CCM ipo Igunga wakati wote (wa uchaguzi na usio wa uchaguzi). Vyama vya upinzani huonekana kule tu wakati wa uchaguzi,” alisema Nape na kuongeza kwamba hiyo ndiyo sababu inayovifanya vyama hivyo vya upinzani kutumia nguvu nyingi wakati wa uchaguzi.

CCM Wilaya, mkoa kuongoza mashambulizi

Alisema tofauti na vyama vya upinzani, katika uchaguzi wa Igunga, CCM Mkoa wa Tabora na Wilaya ya Igunga ndio watakaosimamia kampeni za chama hicho.

Nape alisema hali hiyo ni tofauti na vyama hivyo vya upinzani ambavyo huhamishia viongozi wake wote wa kitaifa kwenye chaguzi ndogo ili kujenga nguvu.

“Vyama vya upinzani wao huhamishia viongozi wake wote wa makao makuu hadi walinzi wa ofisi ili kupiga kampeni,” alidai.

Aliongeza,  “Sisi hatuna haja hiyo. Kama akiwepo kiongozi wa juu, anakuwa anapita tu. Haendi kuweka kambi.”

Alisema kiongozi wa ngazi za juu kabisa anayeweza kuwepo kwenye kampeni za CCM Igunga kwa muda wote ni Katibu wa Uchumi na Fedha, Mwigulu Nchemba ambaye ni mlezi wa chama hicho Wilaya ya Igunga.

Hata hivyo, ingawa Nape ametoa sababu hizo za kuachia uongozi wa wilaya na mkoa, lakini moja ya mambo yaliyojadiliwa kwenye CC iliyoketi mjini Dodoma mwezi uliopita ilimpiga marufuku katibu huyo na baadhi ya makada wake wenye mlengo kama wake kutoshiriki kampeni hizo kutokana na hali halisi ya siasa za makundi ndani ya chama hicho.

Uamuzi huo wa CC ulilenga kuepusha uwezekano wa CCM kulipoteza jimbo hilo endapo baadhi ya watu waliokuwa wakimshambulia Rostam kama wangeshirikishwa kwenye kampeni za uchaguzi huo na kuondoa umoja na mshikamano.   

CCM kutumia helikopta

Kwa mujibu wa Nape,  CCM itaingia katika uchaguzi kwa kutumia helikopta kutokana na  jiographia ya jimbo hilo.

“Tunaenda kuwaeleza historia ya jimbo hilo, tumetoka wapi, tupo wapi na tunaenda wapi,” alisema Nape na kuongeza hilo litandamana na jinsi utekelezaji wa sera za CCM umefanyika kwenye jimbo hilo.

MWANANCHI

No comments: