ANGALIA LIVE NEWS
Tuesday, August 30, 2011
CAG: Sina hofu ya uchunguzi wa Bunge kwa Jairo
Ramadhan Semtawa
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh amesema hana hofu juu ya uchunguzi unaotarajiwa kufanywa na Kamati ya Bunge kuhusiana na tuhuma za Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo.
Kauli hiyo ya kwanza ya Utouh imekuja wakati Kamati hiyo teule iliyotangazwa na Spika, Anne Makinda Ijumaa iliyopita inatarajiwa kuanza kukutana Jumatatu ijayo.
Huku uchunguzi huo mpya wa Bunge unaotarajiwa kuchukua wiki nane ukiibua mjadala mzito nchini kwa watu wa kada tofauti wakiwamo wasomi, CAG Utouh alisema hana shaka nao kwani kila upande unafanya uchunguzi kwa kutumia hadidu zake za rejea.
CAG Utouh alisema ofisi yake ilipewa hadidu zake za rejea ambazo ilizitumia kufanyia uchunguzi huo hivyo haoni tatizo lolote kama Bunge nalo litafanya kwa kutumia hadidu zake za rejea.
Julai 21, Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo alitangaza kumpa CAG siku 10 kufanya uchunguzi dhidi ya tuhuma za Jairo zilizoibuliwa bungeni mnamo Julai 18, mwaka huu wakati wa mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka 2011/12.
Luhanjo katika agizo hilo alitoa hadidu 15 za rejea kwa CAG.
“Watu waende kwa Luhanjo wakaangalie kwanza hadidu za rejea za ule uchunguzi wetu na hizo za Bunge. Kama bunge linafanya uchunguzi wake litatumia hadidu zake za rejea, kwa hiyo jambo la msingi ni kusubiri matokeo ya uchunguzi huo,” alisema Utouh.
Utouh alisema bahati nzuri, moja ya hadidu za rejea za uchunguzi huo wa Bunge ni kupitia ripoti ya uchunguzi uliofanywa na ofisi yake na kuongeza: “Nikisema sana maana yake nitaharibu au kuingilia mchakato huo kwa sababu watapitia na ripoti yangu.”
CAG aliongeza kwamba kitu cha msingi ni kusubiri matokeo hayo ya Bunge yatakapotoka ili kuona undani wa jambo hilo na kusisitiza, “Tusijadili sana uchunguzi huo.”
Alipoulizwa kwamba haoni kama uchunguzi huo mpya wa Bunge unaweza ukaitia doa ripoti ya uchunguzi wa ofisi yake Utouh alijibu: “Ndiyo maana, nasema sitaki kujadili sana maana nisije nikaingilia matokeo ya uchunguzi wa bunge, tusubiri wamalize na tuone matokeo.”
Uchunguzi wa CAG
Awali, Agosti 23, mwaka huu akisoma matokeo ya uchunguzi huo Ikulu akiwa amefuatana na Luhanjo, Utouh alisema pamoja kuandikiwa barua ya kufanya uchunguzi alipewa hadidu za rejea 15 kama mwongozo wa kufanya uchunguzi huo.
“Kazi hii ya uchunguzi ilihusisha vitabu na risiti, hati za malipo na taarifa za benki kwa kipindi cha Mei hadi Julai, 2011. Timu ya ukaguzi iliwahoji watu mbalimbali kutoka taasisi zilizochangishwa, wizara, wabunge na Wakala wa Jiolojia Tanzania(GST),” alisema Utouh.
Alisema ukaguzi ulibaini kuwa idadi ya taasisi zilizopelekewa barua za kuchangia gharama za kuwasilisha bungeni bajeti ya Wizara ni nne na siyo 20 kama tuhuma zilivyodai.
Alizitaja taasisi hizo kuwa ni Rural Energy Agency (REA), Tanesco, TPDC, Ewura, Idara ya Uhasibu na Idara ya Mipango ya Wizara ya Nishati na Madini ambazo zilichanga jumla ya Sh149,797,600.
Alisema ukaguzi maalumu haukupata ushahidi wowote wa fedha zilizochangwa kutumika kuwalipa wabunge ili bajeti hiyo ipitishwe kirahisi.
CAG alisema kwamba ilibainika kwa uhakika kuwa malipo yaliyofanyika yalihusu posho ya kujikimu na posho za vikao kwa maofisa walioshiriki katika shughuli nzima ya kuwasilisha bajeti ya wizara na kwamba hakuna ushahidi wa malipo kwa wabunge.
Utouh alisema mpaka siku ya ukaguzi, Julai 29, mwaka huu akiba ya fedha zilizochangwa kwa ajili ya kuiwasilisha bajeti bungeni ilikuwa Sh195,235,567.33. Alisema Sh20milioni ni akiba ya fedha za matumizi ya fedha zilizochangwa na kupokelewa kwenye akaunti ya GST kabla ya kufanyika marejesho ya Sh99,438,380 na Sh14,860,000.
Hadidu rejea za Kamati ya Bunge
Akitangaza kamati hiyo inayoundwa na Wabunge, Ramo Makani, Tunduru Kaskazini (CCM), Gosbert Blandes, Karagwe (CCM), Mchungaji Israel Natse (Karatu-Chadema), Khalifa Suleiman Khalifa (Gando-CUF) na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Martha Umbulla, Spika Makinda alisema itafanya kazi kwa kuongozwa na hadidu tano za rejea.
Alizitaja kuwa ni kuchunguza utaratibu uliotumika wa kukusanya fedha kwa ajili ya kukamilishwa kwa uwasilishaji wa hotuba za bajeti za wizara bungeni na kwamba, hadidu hiyo ya kwanza itakuwa na vipengele vitatu.
Vipengele hivyo ni pamoja na kuchunguza uhalali wa utaratibu huo kisheria na kwa mujibu wa kanuni, iwapo fedha hizo huwa zinakasimiwa katika bajeti husika pamoja na matumizi halisi ya fedha zilizokusanywa.
Hadidu rejea ya pili ni kupitia taarifa ya CAG kuhusu uchunguzi alioufanya kuhusiana na agizo la Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha fedha taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kwa ajili ya kufanikisha uwasilishaji wa Bajeti ya Wizara hiyo Bungeni.
Hadidu rejea ya tatu, ni kuchunguza mfumo wa Serikali kujibu hoja zinazotolewa bungeni na taratibu za kuarifu Bunge matokeo ya utekelezaji wa hoja hizo.
Makinda alisema hadidu rejea hiyo ya tatu ina vipengele viwili ambavyo ni kuchunguzwa kwa usahihi wa utaratibu uliotumiwa na Katibu Mkuu Kiongozi kwa suala la Jairo na kubaini iwapo utaratibu huo umeathiri dhana ya haki, kinga na madaraka ya Bunge.
Hadidu rejea ya nne, ni kuangalia nafasi ya mamlaka ya uteuzi kwa ngazi za makatibu wakuu katika kushughulikia masuala ya nidhamu ya anaowateua na ya mwisho inawaelekeza wajumbe wa kamati hiyo kuangalia mambo mengine yoyote yenye uhusiano na uchunguzi huo.
MWANANCHI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment