Joyce Joliga
WATU sita wameteketea kwa moto na kubaki majivu baada ya gari walilokuwa wamepanda aina ya Land Rover kuacha njia na kuingia kwenye korongo kisha kuwaka moto.Tukio hilo lilitokea juzi saa 12:00 jioni katika Kijiji cha Chunya karibu na mji mdogo wa Mbamba Bay, wilayani Mbinga na watu hao hawajafahamika hata jinsi zao.
Kamanda wa Polisi wa Ruvuma, Michael Kamuhanda alisema gari aina ya Land Rover 110 lilikuwa likiendeshwa na dereva, Stephen Ngoko (32).
Kamanda Kamuhanda alisema gari hilo lilikuwa likitokea Mbinga kwenda Mbamba Bay na kwamba abiria wawili walijeruhiwa na wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mbuyula.
Aliwataja majeruhi hao kuwa ni Jeremia Masalo (39), Mtanzania anayeishi Msumbiji pamoja na mtoto Anna Geofrey (3), mkazi wa Mbinga.
Akizungumza hospitalini hapo, Masalo alisema gari walilokuwamo lilikuwa na tatizo la breki na ndani yake lilikuwa limebeba madumu zaidi ya 20 petroli. Alinusurika baada ya kupasua kioo kwa kupiga kichwa na ngumi na kutoka huku akiwa ameungua vibaya katika sehemu ya makalio na mikononi na hawezi kutembea.
Alisema kondakta wa gari hilo aliruka kutoka juu alipokuwa baada ya kupinduka.
Kamanda Kamuhanda alisema kondakta alikuwa akijitahidi kuwaokoa abiria wengine kwa juu ya gari, alipokuwa amepanda na kufungua mlango.
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Mbinga, Sebastian Muhikwa alisema Jeremiah ameungua miguuni, kiunoni pamoja na makalio hivyo anatibiwa akiwa amelala.Dereva wa gari hilo anadaiwa kuwa alikimbia baada ya ajali na anatafutwa na Polisi.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment