ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 8, 2011

CCM waanza kulia faulo mbio za kumrithi Rostam


Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye
Hastin Liumba, Igunga
SIKU chache baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kutangaza mchakato wa kumpata mrithi wa Rostam Aziz katika Jimbo la Igunga, CCM imeanza kulalamikia kile ilichokiita mchezo mchafu wa Chadema kuanza kampeni kwa kutumia kete ya njaa inayowakabili baadhi ya wananchi jimboni humo.Kilio cha CCM kinakuja kipindi ambacho Chadema nayo juzi kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Dk Willibrod Slaa kimelalamikia Nec kutokana na kile ilichokiita mkakati wake wa kukibeba chama tawala katika uchaguzi huo mdogo.

Juzi, Dk Slaa alikaririwa na gazeti moja la wiki (siyo Mwananchi Jumapili) akituhumu kwamba, Kamati Kuu (CC) ya CCM ilijadili ratiba ya uchaguzi huo wa Igunga kabla ya Nec kutangaza rasmi, hali inayoonyesha vyama hivyo vya upinzani vilizungukwa.

Wakati Dk Slaa akirusha tuhuma kwa Nec kwamba ilivizunguka vyama vingine kwa kutoa ratiba ya uchaguzi huo kwa chama hicho kinyemela, CCM nacho kupitia kwa Mwenyekiti wake wa Mkoa wa Tabora, Hassan Wakasuvi kimeonyesha hofu kwa Chadema kwa kutumia tatizo hilo la njaa kama mtaji na kete muhimu kisiasa.

Wakasuvi alisema jana kwamba licha jimbo hilo kuwa wazi hadi sasa baada ya Rostam kujiuzulu Julai 13, mwaka huu kampeni hazijaanza lakini akaelezea kushangazwa kwake na baadhi ya viongozi wa Chadema kuanza kupita maeneo yenye njaa kufanya kampeni za chini kwa chini na kukiuka kanuni, sheria na taratibu za uchaguzi.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, viongozi hao wamekuwa wakitumia majukwaa na kuanza kusema kuwa CCM kimeshindwa hata kuwasaidia wananchi wenye njaa katika baadhi ya maeneo wakidhani kuwa ni huo ni mtaji wa kisiasa.

Alisema yote yaliyofanywa na Rostam katika kipindi cha miaka 18 yataendelezwa kwa kishindo huku akisisitiza kuwa tatizo la njaa linashughulikiwa na kwamba kamwe jimbo hilo halitaangukia mikononi mwa wapinzani."Chama kitasimamisha mtu ambaye ni dhahiri atakubalika kwa wananchi na ataendeleza yote mazuri yalifanywa na Rostam katika kipindi cha miaka 18 iliyopita na kamwe hakuna mbadala wake," alisema.

Alisema uchukuaji fomu kwa wanaCCM wanaotaka kuwania kiti hicho utaanza wiki ijayo na kuwataka wanachama wenye sifa kujitokeza.
Wakasuvi alitupilia mbali madai kwamba chama chake kipo hoi katika jimbo hilo akisema hayo ni maneno ya mitaani na kuwataka wale wote wenye kukitilia shaka kusubiri muda utakapofika waone jinsi kitakavyoshinda na kuwaacha midomo wazi.

Tambo za katibu
Katibu wa CCM Mkoa wa Tabora, Idd Ame amejigamba kwamba kelele za wapinzani kamwe haziwezi kuwanyima usingizi akisema chama chake kitafanya kampeni za kistaarabu na kisayansi na kwamba wanaoanza kampeni kabla watachapwa muda ukifika.
"Nani anasema sisi tuko hoi Igunga... siyo kweli hatutishiki na hizo bendera, ieleweke wazi kuwa muda ukifikia CCM itashinda kwa kura nyingi," alisema Ame.

Tayari CCM kupitia kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye kimeshatangaza mchakato wa utoaji wa fomu kwa wanachama wanaotaka kuwania nafasi hiyo kuanzia kesho hadi Jumamosi ijayo.

Mwananchi

No comments: