Advertisements

Tuesday, August 9, 2011

Chadema yatangaza ratiba ya Igunga, CCM nao waanza kuchukua fomu leo


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza ratiba ya mchakato wa kumpata mwanachama atakayesimamishwa kugombea ubunge katika Jimbo la Igunga, mkoani Tabora, ambaye kimesema atateuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mdogo jimboni humo, Agosti 20, mwaka huu.

Tayari Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imekwishakutangaza tarehe ya uchaguzi huo, ambao utafanyika Oktoba 2, mwaka huu, huku Chadema kikiwa chama cha pili kutangaza ratiba yake hiyo, ikitanguliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiliyotangaza wiki iliyopita.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, Erasto Tumbo, alisema kupitia tamko la chama hicho jana kuwa uamuzi wa kushiriki uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo hilo, ni katika maazimio yaliyofikiwa na Kamati Kuu ya chama katika kikao chake kilichofanyika mjini Dodoma, Agosti 6, mwaka huu.Kutokana na hilo,
amewataka wanachama wenye nia na sifa ya kugombea ubunge katika jimbo hilo, kujitokeza kuchukua fomu za chama kuanzia kesho. Alisema mwisho wa kurudisha fomu hizo, utakuwa Agosti 16, mwaka huu, saa kumi kamili jioni.
Tumbo alisema baada ya hapo, Agosti 17, utafanyika uchujaji wa majina ya wagombea na Agosti 18 Mkutano Mkuu wa Wilaya utapiga kura kwa majina hayo. Alisema Agosti 19 Kamati Tendaji ya Wilaya itapokea majina na kuweka alama kwa kila mgombea.
“Hatimaye 20/8/2011 Kamati Kuu itakutana Igunga kwa ajili ya uteuzi wa mwisho, ambapo mgombea wa Chadema atapatikana na tayari kwa harakati za kampeni,” alisema Tumbo.
Uchaguzi mdogo katika jimbo hilo, unafanyika kutokana na kujiuzulu kwa aliyekuwa mbunge wake, Rostam Aziz.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa (CCM), Nape Nnauye, alisema wanachama wa chama hicho wataanza kuchukua fomu kuanzia leo hadi tarehe 15. Alisema tarehe 15 kura za maoni zitaanza na kufuatiwa na kikao cha kamati ya siasa ya wilaya, kamati ya siasa ya mkoa, sekretarieri na kisha Kamati Kuu.
“Tarehe rasmi za kuteua jina hazijathibitishwa hivyo siwezi kuzitaja ila tuna uhakika zitaendana na ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),” alisema Nnauye.
CHANZO: NIPASHE

No comments: