Advertisements

Tuesday, August 9, 2011

Barrick yasafirisha wabunge wakaikague


Ni Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira
  Yatoa ndege tatu kutoka Dodoma hadi North Mara
  Wanafuatilia sakata la uchafuzi mto Tigithe
Mgodi wa North Mara Barrick
Wabunge wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, wamekwenda mgodi wa North Mara Barrick, uliopo Nyamongo wilayani Tarime mkoani Mara kukagua utekelezaji wa maagizo ya kamati hiyo, wakitumia ndege zilizokodiwa na mgodi huo.
Safari ya wabunge hao iliyofanyika jana wakitokea Dodoma kwenda Tarime, North Mara na kurejea, ililenga kuangalia mambo yaliyofanyika katika utekelezaji wa maagizo ambayo kamati hiyo ilitoa kwa mgodi huo mwaka 2009, walipoutembelea.
Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli, ilitua kwa ndege saa 5:00 asubuhi.

Mwaka 2009 mto Tigithe unaotumiwa na baadhi ya wakazi wanaouzunguka mgodi huo uliathiriwa na tindikali iliyovuja kutoka mabwawa ya kuhifadhi maji, baada ya kufanyika kwa wizi wa maturubali ya kuzuia maji kuvujia ardhini.
Pia uvujaji wa tindikali hiyo, ambayo hujitengeneza kiasili kutokana na mawe yaliyochimbwa ardhini kunyeshewa na mvua, ulisababishwa na rundo la mawe hayo ambayo yaliachwa bila kuhamishwa baada ya kuondolewa dhahabu, ilitiririka hadi mtoni.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, James Lembeli, alisema mwaka 2009, kamati yake ilifanya ziara katika mgodi huo kuangalia matatizo yaliyopo katika mgodi huo.
Alisema safari ya jana ililenga kuangalia mambo yaliyofanyika katika utekelezaji wa maagizo waliyoyatoa wakati walipotembelea mgodi huo mwaka 2009.
Alipoulizwa kuhusu nani aligharimia safari hiyo, Lembeli alisema jambo hilo halihusiani na madhumuni ya ziara hiyo.
Alisema mgodi huo, uliandika barua kuwaeleza kuwa wameyakamilisha na kuwataka waende huko.
Kumekuwa na taarifa ambazo hata hivyo zilikanushwa na Lembeli kuwa mara baada ya ugeni huo kuwasili, wenyeviti watatu wa vijiji vinavyo-zunguka mgodi huo, Elisha Marwa Nyamhanga wa kijiji cha Nyangoto, Omtanzania Omtima wa kijiji cha Kewanja na mwenyekiti wa kijiji cha Matongo, Daudi Itembe na baadhi ya wazee wa maeneo hayo waliokuwa na shauku ya kuingia na kuzungumza na wageni hao, lakini walizuiwa kuingia mgodini.
Mbali na viongozi hao, pia Mbunge wa Jimbo la Tarime, Nyambari Nyangweni (CCM), naye alialikwa kuungana na wajumbe wa Kamati hiyo kwenda Tarime kupata uhakika wa mambo yanayoleta mgogoro kati ya wananchi na kampuni hiyo, lakini akajiondoa dakika za mwisho.
Ilielezwa kuwa mbunge huyo alipofika uwanja wa ndege na kukuta wabunge hao wanasafiri kwa kutumia ndege ya kampuni hiyo alisita kupanda na kuwaacha wabunge wenzake.
Alipotafutwa kuzungumzia sakata hilo, Nyambari Nyangwine alisema: “Mimi nimekataa kuungana na wabunge wenzangu wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kuja huko kwa kuwa kampuni ya Barrick ndiyo inatuhumiwa na wapiga kura wangu …. Wanawanyanyasa kwa kutowalipa fidia za mali zao hadi sasa mbali na kuwahamisha katika maeneo yao,” alisema.
Alisema kumekuwa na madhara makubwa kwa wananchi kutokana na matumizi ya maji yenye kemikali ya sumu kutoka maeneo ya mgodi huo na kuingia mto Tigithe.
“Hivi karibuni nilitoa kilio changu hapa bungeni kuhusu madhara na unyanyasaji unaofanywa na kampuni hiyo dhidi ya wapiga kura wangu, leo hii tena wanione nateremka kutoka kwenye ndege ya mgodi huo si watanishangaa,” alisema.
Alisema serikali ina uwezo wa kuwasafirisha wabunge wa Kamati yoyote kama kuna suala lenye mgogoro ambalo linahitaji ufumbuzi.
Lembeli akizungumzia habari za kuzuiwa viongozi wa vijiji na wazee kuingia mgodini alisema: “huo ni uwongo hapa tulipo tupo na mwenyekiti wa kijiji cha Nyamongo.”
Alisema katika kamati yake kuna wajumbe pia kutoka kambi ya upinzani na alimtaja mmojawapo kuwa ni Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.
Alisema pia katika msafara huo, walikuwepo watu wanaotunza kumbukumbu za Bunge na maofisa habari wa Idara ya Maelezo.
Kuhusu Mbunge wa jimbo la Tarime Nyangwine kukataa kuambatana nao kwa madai kuwa mwaliko huo una harufu ya rushwa, Lembeli alisema kuwa mbunge huyo alikataa kwa sababu zake mwenyewe.
Alisema pia si mjumbe wa kamati yake na kwamba hata wakati kamati hiyo inatembelea mwaka 2009, Nyangwine hakuwepo kwa sababu hakuwa mbunge.
Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel, alisema kuwa kamati hiyo ilikwenda kwa ziara ya kawaida ya kikazi na kwamba safari hiyo haikugharimiwa na Bunge.
Meneja Uhusiano wa Barrick, Teweli Teweli, alisema ni kweli wabunge hao walikwenda katika mgodi huo kwa ajili ya kuangalia kama maagizo ya mwaka 2009 yametekelezwa.
Alisema mwaka huo ilitolewa amri ya kulinda mazingira (environment protection Order) na ili amri hiyo iondolewe lazima ukaguzi ufanyike.
Teweli alisema ukaguzi huo hufanywa na Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Kamati ya Bunge inayohusika na mazingira.
“Kwa mujibu wa sheria anayekaguliwa ndiye anatakiwa kulipa gharama zote kwa wajumbe wanaokwenda kukagua, hivyo kwa kuwa wale ni wabunge na wanaendelea na vikao mjini Dodoma imeonekana ni busara waende na kurudi Dodoma,” alisema.
Hata hivyo, Teweli hakusema ni ndege ngapi zilitumika kuwabeba wabunge hao na wajumbe wengine waliofuatana nao.
“Sina uhakika na idadi ya ndege zilizowabeba kwa kuwa sikuwa kule mimi, ila nikishazungumza na bosi wangu nitawajulisha,” alisema Teweli.
Wakati Teweli akisema hivyo, habari ambazo NIPASHE imezipata ni kwamba Barrick ilitumia ndege tatu zilizowapeleka wabunge mgodini.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Mh. Lucas, sijui kama ni jukumu lako kusimaia uthibati wa ujmbe unaoingia kwnye ukumbe wetu wa vijimambo. Nasema hivi ni kwa shaka ya taarifa za jumla za ndege zilizotolewa kwenda mara kuchunguza sualala mgodi. Kama kweli ni ndege tatu zilizotolewa kwa kazi hiyo, ni tatizo kuba sana la matumizi ya mali ya umma. Ni matumaini yangu taarifa hizi za jumla ya ndege zimekosewa, ili tuwalinde na kuwapongeza wale wanaofanya kazi za umma au za jamii.