Advertisements

Tuesday, August 9, 2011

HASARA ZA WATOTO KIMAPENZI KWENYE NDOA!

NIANZE kwa kumshukuru Muumba wa mbingu na nchi, kwa wema anaonifanyia maishani mwangu.
Baada ya utangulizi huo, sasa tuingie moja kwa moja kwenye mada yetu  ya leo kama inavyosomeka hapo juu.
Yaweza kuwa imekushitua sana lakini ukweli utabakia palepale kwamba kuna hasara za watoto kimapenzi katika ndoa, vipengele vifuatavyo vinabeba hoja nzito katika kudhihirisha jambo hili.

HUTEKA MAPENZI!
Ni wazi kuwa wanandoa wanapokuwa bado hawajapata watoto, hufanyiana mambo mengi sana ya kimapenzi kama kuleteana zawadi, kupendelea  kukaa pamoja kwa muda mrefu na kuonjeshana kila  aina ya upendo wa dhati.


Lakini hali hii hubadilika pindi wanapopata watoto, kwani sehemu kubwa ya mapenzi yao huhamishia kwa watoto.
Wazazi huanza kuwajali zaidi watoto na kujisahau, hivyo mapenzi hupungua siku hadi siku. Hali hii huchukua nafasi kubwa zaidi kwa akina mama ambao hufikia hadi hatua za kupunguza kama si kusitisha kabisa baadhi ya huduma za muhimu kwa waume zao.

Mfano, labda mama alikuwa na kanuni ya kumnawisha mikono mumewe kabla ya kula, kumvalisha nguo wakati wa kulala nk, lakini pindi wanapoanza kupata  watoto huduma hizi sasa husitishwa na huhamishiwa kwa watoto.
Hivyo basi, uwepo wa watoto kwenye ndoa, huteka mapenzi ya wazazi wao na kuondoa kabisa ile morali ya mapenzi kwa wanandoa hasa wasipokuwa makini.

HUCHOCHEA MIGOGORO!   
Hapa naomba nieleweke kwa undani kuwa, watoto huchochea migogoro mingi sana kwenye ndoa, huku pointi muhimu katika hoja hii ikiwa ni kutofautiana kwa wazazi katika suala zima la malezi kwa watoto.

Kama nilivyowahi kueleza huku nyuma kuwa, wanandoa wamekulia kwenye mila, tamaduni na malezi tofauti ya kifamilia, hivyo basi wanapokuwa wamepata watoto, hapo kila mmoja hutaka kuwafundisha watoto maadili ambayo anayajua yeye bila kujali utofauti wa maadili hayo kwa mzazi mwenzake. Hapo ndipo migogoro huibukia.

Mfano, baba anamkataza mtoto kufanya jambo fulani ambalo yeye anaamini kuwa si njema,  wakati huohuo, mama anaamini kuwa jambo hili si baya, ghafla majibizano na mitafaruku huweza kutokea.

Itaendelea wiki ijayo.

www.globalpublishers.info

No comments: