ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, August 18, 2011

Ikibidi, mpenzi wako asiguse kabisa simu yako!

TUNAKUTANA tena kupitia safu hii nikiamini umzima na unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku kama kawaida. Kwa Waislam najua swaumu kama kawa, Mungu awajaalie afya njema na mmalize salama salmini.

Ndugu zangu, huko nyuma niliwahi kuandika namna simu za mkononi zinavyovuruga uhusiano. Tatizo la wapenzi na wanandoa kukorofishana mara kwa mara kutokana na kushutumiana juu ya utumiaji mbaya wa simu zao za mkononi si geni kwa walio wengi.


Walioachana kwa sababu ya chombo hicho cha mawasiliano ni wengi lakini pia wale ambao ‘wanatifuana’ kila kukicha kila mmoja akimfikiria mwenzake tofauti kuhusiana na matumizi mabaya ya simu yake idadi ni kubwa kuliko maelezo.


Kwa maana hiyo basi, leo nataka kuzungumzia kitu ambacho naweza kutofautiana na wengi lakini ndiyo ukweli hasa katika kipindi hiki, lengo ni kuleta amani na kuwafanya wapenzi na wanandoa kudumu muda mrefu bila migogoro isiyokuwa na lazima.

Juzi nilipata simu kutoka kwa msomaji wangu mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Suzan wa Arusha. Katika maelezo yake anadai ameachwa na mume wake baada ya mwanaume ambaye alikuwa mpenzi wake wa zamani kuanza tabia ya kumpigia simu usiku na wakati mwingine kumtumia sms kuonesha bado wanaendelea kupeana mambo.

“Inaonekana ni tabia ya baadhi ya watu kufanya makusudi ya kugombanisha wanandoa au wapenzi ili waachane, sijui wanapata faida gani. Nilimpa uhuru mume wangu kuishika simu yangu wakati wowote, kilichonipata ni kuachika.

“Kuna mwanaume siku moja alinitumia sms akinipongeza kwa penzi nililompa jana yake, kitu ambacho hakina ukweli. Kwa bahati mbaya siku hiyo nilimuaga mume wangu kuwa naenda kumtembelea shangazi huko Moshi. Sikumjali lakini kosa nililofanya sikuifuta ile sms.

“Mume wangu akaiona na kunipa kibano cha hali ya juu. Nilijaribu kumwambia ukweli wa mwanaume huyo lakini sijaeleweka na mbaya zaidi tukiipiga ile simu haipatikani. Tukawa hatuaminiani kabisa, mume wangu akawa anahisi namsaliti.

“Hivi ninavyoongea na wewe sina ndoa. Mume wangu kaniacha kwa sababu ya kumpa uhuru kushika simu yangu,” alisema Suzan.

Tunajifunza nini kwa ushuhuda huu? Wewe haijawahi kukutokea hii? Jitu linakutumia sms hulijui lakini linakuambia linakupenda sana kuliko hata mumeo anavyokupenda, mumeo akiiona hii atakufikiriaje? Ni sawa unaweza kumuelewesha lakini je, kama huyo mpenzi wako ni mgumu wa kuelewa unadhani nini kinaweza kutokea hapo?

Nilishawahi kusema kwamba, ili kumjengea mpenzi wako mazingira ya kukuamini, mpe uhuru wa simu yako lakini ukweli ni kwamba uhuru huo huo niliouzungumzia ndiyo unaosababisha matatizo kwa walio wengi leo hii.

Ndiyo maana baadhi ya watu wanasema kama ni kutokuaminiwa na wenza wao bora iwe hivyo lakini hawawezi kuwapa uhuru wa kushika simu zao, kwa nini? Kwa kuwa wanajua watatibuana kila mara.

Unaweza kumfikiria mpenzi wako tofauti kwamba anaficha madhambi yake kwa kukukataza kugusa simu yake lakini wakati mwingine yawezekana ni katika kuepusha matatizto na wala hakuna uovu wowote unaofichwa. Itaendelea wiki ijayo.

www.globalpublishers.info

No comments: