ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 8, 2011

Kashfa UDA yatinga kwa Polisi, TAKUKURU



Godfrey Ismaely,Dodoma na Tumaini Makene


Wabunge Dar es Salaam wachachamaa
*Idd Simba azungumzia kilichotokea

SERIKALI imemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG, Mkurugenzi mkuu wa Makosa ya Jinai (DCI) na Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya uchunguzi wa kina juu ya kashfa ya uuzaji wa Shirika la Usafirishaji Dar es Salaam (UDA) ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya viongozi waliohusika.


Tamko hilo lilitolewa jana na Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda bungeni mjini Dodoma wakati akitoa taarifa fupi kwa wabunge kabla ya kuendelea na kipindi cha maswali na majibu.


“Suala jingine lililoongelewa kwa hisia kali na waheshimiwa wabunge wengi wakati wa mjadala ni matatizo ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam, Mheshimiwa spika serikali imesikia kilio hicho cha waheshmiwa wabunge,” alisema Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda na kuongeza:

“Kwa sasa, serikali imewaagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya uchunguzi wa kina na kuwasilisha taarifa serikalini mapema iwezekanavyo.”

Waziri Mkuu alisema kuwa mara baada ya uchunguzi huo kukamilika wahusika wote watachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Baada ya uchunguzi kukamilika, serikali itachukuwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu kwa wote watakaobainika kuhusika kulihujumu shirika hilo,” alisema Bw. Pinda.

Wakati huo huo wabunge wa Dar es Salaam jana wakiongozwa na mwenyekiti wao Bw. Abbas Mtemvu (Temeke-CCM) walizungumza na  waandishi wa habari mjini Dodoma na kueleza kusikitishwa na tuhuma za ufisadi, ukiukwaji wa sheria, kanuni, taratibu na maslahi ya wananchi katika mchakato wa ubinafsishaji wa UDA.

“Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam tunamshukuru Waziri Mkuu kwa taarifa na ufafanuzi alioutoa bungeni Agosti 4, mwaka huu, ambapo aliagiza vyombo vya dola hususan, TAKUKURU, CAG na DCI kufanya uchunguzi kuhusu tuhuma husika, tupo tayari kutoa ushahidi kwa vyombo hivyo pamoja na kushirikiana na serikali ili hatua stahiki zichukuliwe,” alisema Bw. Mtemvu.

Wabunge hao ni pamoja ni Bw. Mtemvu, Bw. John Mnyika (Ubungo), Bw. Mussa Zungu (Ilala), Dkt. Faustine Ndungulile (Kigamboni), Bw. Idd Azzan (Kinondoni), Bi. Eugen Mwaiposa (Ukonda), Bi. Halima Mdee (Kawe), Dkt. Makongoro Mahanga (Segerea) na wengine wa viti maalumu akina Philipa Mturano, Mariam Kisangi, Zarina Madabida, Ester Bulaya, Angellah Kairuki na Fanella Mkangara.

Wabunge hao walisema kuwa pamoja na vyombo vya dola kuagizwa kufanya uchunguzi kwa UDA pia wanatoa wito kwa serikali kuagiza kusitishwa mara moja mkataba batili uliofanyika awali.

“Wabunge wa jiji la Dar es Salaam tunatoa wito kwa serikali kuagiza kusitishwa mara moja kwa mkataba batili na maamuzi haramu yaliyofanyika kwa kukabidhi hisa, mali, uendeshaji wa UDA kwa kampuni ya Simon Group Limited ili katika kipindi hiki cha uchunguzi masuala yote ya kampuni hiyo yaratibiwe na Bodi huru itakayoundwa na kusimamiwa na Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) kwa mujibu wa sheria zinazohusika,” alisema Bw. Mtemvu.

“Pia tunataka Meya Massaburi, Mkurugenzi wa Jiji, Bw. Bakari Kingobi na watendaji wote wa jiji la Dar es Salaam walihohusika wasimamishwe  mara moja katika kipindi chote cha uchunguzi na kuchukuliwa hatua stahili baada ya uchunguzi huo kwa mujibu wa sheria, kanuni na maslahi ya umma, aida hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa mwenyekiti wa bodi ya UDA, wajumbe wote wa bodi na watendaji wote walihohusika na kashfa hiyo,” aliongeza.

Iddi Simba ajibu tuhuma dhidi yake

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa kampuni hiyo, Bw. Idd Simba amejibu tuhuma zilizoelekezwa kwake, akisema mchakato wote ulikwenda kwa mujibu wa taratibu na sheria za nchi, akisema serikali ilijulishwa kila hatua.

Huku akitoa madai ya kughushiwa kwa saini ya Meneja wa UDA, Bw. Victor Milanzi kuonesha kuwa mnunuzi alielekezwa kuweka fedha katika akaunti binafsi, Bw. Simba alisema kuwa kutokana na mchakato wa uuzwaji wa UDA kufuata sheria na taratibu za nchi kadri zinavyojulikana, si sawa kusema kampuni hiyo imemilikisha hisa zake isivyo halali wala kuwa imetapeliwa fedha zake.

Akizungumza na Majira juu ya sakata hilo, hasa tuhuma kuwa alipokea sehemu ya malipo ya ununuzi na fedha hizo kwenye akaunti yake binafsi, Bw. Simba alisema kuwa fedha hizo hazihusiani na ununuzi na uuzwaji wa UDA, bali masuala mengine kati yake na Simon Group Ltd.

Bw. Simba ambaye amewahi kuwa kiongozi mwandamizi serikalini, alisema kuwa taarifa za mchakato wote wa uuzwaji wa UDA alikuwa akiziwasilisha serikalini, kwa Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi na kwa Kampuni Hodhi ya Mashirika ya Umma (CHC).

Alisema kwa mujibu wa kanuni za UDA, madaraka ya uuzaji wa hisa ambazo hazijagawiwa yako mikononi mwa bodi ya wakurugenzi, ndiyo maana bodi iliendelea na mchakato wa kumuuzia Simon Group kwa mujibu wa sheria na mkataba wa mauzo ukafanyika, huku hisa hizo zikilipiwa, hivyo si kweli kwamba ziliuzwa kiholela.

"Mchakato wote ulikwenda kwa mujibu wa sheria na kanuni. Tulikuwa tunapata ushauri wa wanasheria katika mchakato mzima. Hao wanaodhani na kusema kwamba Simon Group imetapeliwa na kwamba haikumilikishwa hisa za UDA kihalali si sawa, kwani uuzwaji ulifanyika kwa mujibu wa kanuni na sheria tunavyozielewa.

"Kibaya kilichotokea ni kwamba baada ya Simon Group kuhalalishiwa ununuzi wa hisa hizo na kulipia malipo ya kwanza ya milioni 285, mwenyekiti (wa Simon Group), Bw. Robert Kisena akataka kuingia katika utendaji wa kampuni na uongozi wake, hata kabla ya AGM (mkutano wa wanahisa wa mwaka).

"Alipokatazwa kufanya hivyo na kushauriwa kwamba asubiri mpaka taratibu zikamilike, akaingia kwa nguvu kwenye majengo ya kampuni (UDA), kinyume kabisa cha taratibu. Hapo ndipo vurugu zilipotokea. Alipohojiwa hajakamilisha malipo ya pili kama ilivyotakiwa alidai kuna pesa alishalipa katika akaunti yangu mimi Idd Simba, kwa mujibu barua aliyoandikiwa na uongozi wa UDA," alisema Bw. Simba na kuongeza;

"Moja, barua ni ya kughushi, kwa sababu Meneja wa UDA, Milanzi hakuandika barua wala hakukuwa na maagizo yoyote ya yeye kulipia hisa zake kupitia akaunti binafsi. Hilo jambo lisingewezekana.

"Lakini ieleweke kwamba muda mrefu kabla ya tukio hilo na katika shughuli ambazo hazihusiani hata kidogo na UDA, zilizotokana na ushauri wa jumla wa kibiashara aliotaka kutoka kwangu, alikuwa anastahili kulipa fedha zangu binafsi. Nilitoa amri ya kulipia katika akaunti yangu, alifanya hivyo kwa awamu tofauti kadri nilivyotoa maagizo."

Akizungumza mbele ya mwanasheria wake, Bw. Simba alipoulizwa iwapo watu hawawezi kuhoji mgongano wa maslahi ulio wazi katika suala hilo, la Simon Group kununua hisa katika shirika (UDA) ambalo yeye ni mwenyekiti wa bodi, huku pia wakati huo huo yeye akitoa ushauri wa kibiashara kwa kampuni iliyotaka kununua UDA, alisema;

"Ndiyo wanaweza kuhoji...lakini sasa mimi si mtumishi wa umma, pale UDA mimi si mwajiriwa. Mimi nauza maneno, natoa ushauri. Ukija kutaka ushauri siwezi kukutalia. Lakini kwenye bodi tulikuwa serious sana. Tatizo ni kwamba mwanzoni sikutilia maanani sana tabia ya Robert Kisena, kwa sababu mimi nilikuwa na hamu sana mzawa achukue UDA, siyo kila kitu nchi hii anachukua mwekezaji mgeni," alisema Bw. Simba.

Alisema kwamba inasikitisha kuona mpaka sasa serikali haijachukua hatua yoyote kuinusuru UDA, akionesha matumaini yake kwa CHC itachukua hatua za haraka kurejesha hali ya kawaida katika shirika hilo muhimu la usafiri Dar es Salaam, pia kwa kamati iliyoundwa kuchunguza suala hilo.

Wakati Bw. Simba akisema kuwa fedha zilizowekwa katika akaunti yake binafsi hazina uhusiano wowote na uuzwaji wa UDA, Bw. Kisena amenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema kuwa hawakuwahi kuwa na shughuli nyingine tofauti na hiyo ya ununuzi wa shirika hilo la umma.

Akinukuliwa katika moja ya magazeti ya kila siku jana, Bw. Kisena alisema kuwa walilipa fedha hizo katika akaunti ya Bw. Simba, kama sehemu ya malipo ya ununuzi wa UDA, kutokana na maelekezo ya uongozi wa UDA, akisema kuwa anazo nyaraka zinazoonesha hivyo.

No comments: