ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 13, 2011

‘Kuongezewa damu sasa hatari’

World Blood Donation Day Here comes the world day dedicated to blood donation
Fredy Azzah
TAASISI ya kimataifa imesema Watanzania wengi wako kwenye hatari ya kuambukizwa virusi vya ukimwi (VVU) kutokana na kuongezewa damu isiyopimwa kufuatia ukosefu wa vifaa vya kupima virusi hivyo.Kauli hiyo ilitolewa jana mwakilishi wa asasi za kiraia za Mfuko wa Kimataifa wa Kuzuia Ukimwi, Kifua kikuu na Malaria (GFATM), Dk  Peter Bujari alipozungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam.

Dk Bujari alisema upo uwezekano kwa Watanzania wengi kuambukizwa Virusi Vya Ukimwi (VVU) kwa kuongezewa damu kutokana na ukosefu wa vifaa vya kuchunguza usalama wa damu nchini.


Alisema uchunguzi wa asasi hiyo umebaini kuwa mikoa mingi nchini haina vifaa vya kupima ukimwi tangu Januari mwaka huu.“Hali mbaya zaidi ipo kwenye benki za damu, hawana vipimo vya kuhakiki kama damu walizonazo zina virusi ama vipi, juzi tu nimepigiwa simu na benki ya damu Shinyanga wakisema hawana kabisa vifaa hivi,” alisema Dk Bujari.

Alisema katika utafiti huo uliofanywa kwenye wilaya 35 nchini za mikoa mbalimbali  ikiwamo Kilimanjaro, Mbeya, Arusha, Tanga, Shinyanga, Kagera na Mwanza, ni Wilaya ya Kyela pekee iliyokuwa na vipimo hivyo ambavyo hata hivyo vinatarajia kumalizika mwezi huu.Utafiti huo pia ulieleza kwamba, mbali na uhaba wa vipimo  uliopo sasa, hali itakuwa mbaya zaidi mwishoni mwa mwaka huu ambapo hata dawa za kurefusha maisha (ARVs), zitakuwa zimekwisha kabisa kama hatua za haraka hazitachukuliwa.

“Tumepokea taarifa kutoka Wilaya mbalimbali nchini zikisema hazijapata vitenganishi tangu Januari , wilaya moja kati ya 35 ndio inayotoa huduma ambayo nayo inakadiriwa kwamba vitenganishi hivyo vitaisha mwishoni mwa mwezi huu.” alisema na kuongeza:
“Benki ya damu ya Shinyanga haina vipimo kabisa, kukosekana kwa vitenganishi hivi ni hatari zaidi kwa sababu wagonjwa wanaohitaji damu wanaweza kuwekewa damu zenye virusi vya Ukimwi, lakini pia vipimo hivi ni muhimu kwa wajawazito ambao inatakiwa wapimwe virusi vya Ukimwi ili wasiweze kuwaambukiza watoto wao kama wanavyo virusi.”

Dk Bujari ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Human Development Trust (HDT), alisema kufuatia hali hiyo ofisi yake, iliandika barua kwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ili kupata ufafanuzi wa hali hiyo, lakini mpaka sasa hawajajibiwa jambo lolote.“Barua ilipelekwa Agosti 2, lakini mpaka leo hatujajibiwa chochote ndiyo maana tukaamua kutumia vyombo vya habari ili tupate majibu,” alisema Dk Bujari.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Blandina Nyoni alipopigiwa simu ili afafanue mambo hayo alisema yuko kwenye mkutano na kukata simu.Naye Maganga Mkuu wa Serikali Deo Mtasiwa  alipopigiwa simu hakupokea simu iliyoita kwa muda mrefu.

Hata hivyo, Mtafiti  alisema utafiti wao ulibaini pia kuwa  Bohari ya Dawa (MSD), imenunua vidonge  vya kuongeza nguvu kwa waathirika wa Ukimwi (ARVs) ambazo zinakaribia kuisha muda wake kinyume na utaratibu wa kununua dawa hizo.Kwa kawaida dawa hutakiwa kudumu kwa miaka miwili kabla ya muda wake kumalizika, na hutakiwa kuagizwa ikiwa muda wake wa matumizi uliobaki ni zaidi ya asilimia 80.

“Lakini MSD wameagiza dawa Julai 6 mwaka huu na muda wake wa matumizi unamalizika Januari mwakani, zitafanya kazi kwa miezi sita tu, sasa kweli mpaka zifike wilaya ni lini, hii ni hasara kubwa kwa taifa,” alieleza Dk Bujari.

Alisema kuwa dawa zote hizo ziliagizwa kutoka nchini India na zimetengezwa na Viwanda vya Aurobindo, Hetero drugs na Cipla.Mbali ya tatizo hilo, alisema kumekuwa na harufu ya ufisadi katika ununuzi wa dawa hizo kwa kuwa MSD imekuwa ikinunua kikasha kimoja cha ARVs kwa Sh70,500 wakati mpango wa dharura wa Rais wa Marekani wa kupambana na ukimwi (Pepfar), umekuwa ukinunua kikasha kimoja kinacholingana ubora na hizo za MSD kwa Sh30,000 kila kimoja.

Mwananchi

No comments: